Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa amezindua ripoti ya utafiti wa viashiria vya UKIMWI ambavyo inaonesha maambukizi mapya miongoni mwa watu wazima wenye umri Zaidi ya miaka 15 yanaendelea kupungua.
Ameyasema hayo leo Disemba Mosi, 2023 wakati akizungumza na mamia ya wananchi walioudhuria maadhimisho ya siku ya UKIMWI dunia yaliyofanyika kwenye viwanja vya shule ya Sekondari ya Morogoro, Mjini Morogoro.
Amesema kuwa maambukizi mapya miongoni mwa watu wazima wenye Zaidi ya miaka 15 yanaendelea kupungua kutoka watu 72,000 waliokuwepo mwaka 2016/2017 hadi watu 60,000 kwa mwaka 2022/2023 sawa na upungufu wa asilimia 0.18 ambapo asilimia 0.24 ni wanawake na asilimia 0.11 ni wanaume.
Ameongeza kuwa Serikali iliamua kufanya utafiti kwa lengo la kujua hali ya sasa ya VVU na UKIMWI ilivyo hapa nchini na matokeo yameonesha kuwa Tanzania imepata mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya UKIMWI.
Akitoa maagizo mahsusi, Waziri Mkuu amewataka vijana wajitambue na kuthamini Maisha yao kwa kujikinga na maambukizi mapya ya VVU na kuwataka wadau wote kuweka kipaumbele katika kundi hilo muhimu ili kulinusuru na athari za UKIMWI.
Pia amewataka wananchi wanaoishi na VVU waendelee kutumia dawa za ARV kwa ufuasi sahihi bila kuacha ili kufubaza VVU na kuimarisha afya zao ambapo Taifa linawategemea na Serikali itaendelea kuhakikisha huduma za ARV nchini zinapatikana.
Naye Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema kuwa ili kukabiliana na kasi ya kuenea kwa maambukizi wa VVU, wizara ya afya imezindua mpango wa kuoanisha VVU, magonjwa ya ngono na homa ya ini kwani kuna ushabihiano mkubwa wa njia za maambukizi za magonjwa hayo.
Ameongeza kuwa hatua hiyo imekuja baada ya kubaini kuwa asilimia 4.4 ya watanzania wana maambukizi ya magonjwa ya ini. Pia ameeleza kuwa wizara ina mpango wa kufikisha huduma ya afya kwa ngazi ya jamii ambapo wizara hiyo inatarajia kuajiri wahudumu wa afya ya jamii 137,000 ambao watafanya kazi kuanzia ngazi ya mtaa na vitongoji.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa