Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Omari Mgumba amewakumbusha wananchi wote nchini kuwa kilimo ndio uti wa mgongo wa nchi yetu kwani kupitia kilimo watu wanapata mahitaji mbalilmbali ikiwemo chakula, kipato katika kaya, kuongeza mapato ya wilaya na kuinua uchumi wa nchi kwa ujumla, hivyo ni vema kila mmoja akathamini kazi za wakulima kwani ndio tegemeo la chakula kwa taifa letu la Tanzania.
Hayo yamesemwa Oktoba 24 mwaka huu na Naibu Waziri wa Kilimo wakati wa uzinduzi wa msimu wa kilimo 2018/2019 wilayani Kilosa na kuhamasisha wadau wote katika sekta ya kilimo kufanya kazi kwa juhudi kubwa na maarifa katika kuongeza uzalishaji na tija kupitia mnyororo wa thamani kwa kila zao na kuinua kiwango cha ushirikiano kwa hali na mali ili kuinua sekta ya kilimo itakayowezesha wananchi walio wengi kupata kipato na kutoa mchango kwa taifa kuelekea uchumi wa kati ifikapo 2025.
‘‘Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kwa dhati kuboresha sekta ya kilimo na miundombinu ya barabara na reli ya kisasa ambavyo vitasaidia usafirishaji wa mazao na bidhaa hivyo ni rai yangu kwenu kuchangamkia fursa hii kwa kuzalisha mazao ya kilimo kwa wingi pamoja na uwekezaji katika viwanda vya kuchakata mazao ili kuongeza thamani’’. Ameongeza Mgumba
Kaulimbiu ya msimu huu ni kanuni bora za kilimo ndio mkombozi wa mkulima tuzifuate, kwa kaulimbiu hii ni matarajio yangu mtautambua mpango mkakati wa kilimo wa wilaya kasha mtautekeleza kwa kuufanyia kazi ili kuboresha kipato cha kaya, jamii na taifa kwa ujumla kwani wilaya hii ina rasilimali nyingi sana ambazo zikitumika ipasavyo zitaleta maendeleo makubwa katika wilaya na kuondoa hali ya maisha duni kwa wananchi hususan wakulima wadogo.
Aidha Mgumba ametoa wito kwa wakulima kujituma, kubadilika, kujibidiisha, kupokea na kutumia mbinu bora za kilimo na teknolojia zinazotolewa na wataalam kwani miongoni mwa changamoto zinazowakabili wakulima ni kutozingatia kanuni bora za kilimo pamoja na hivyo wakulima hao wanapaswa kuzingatia kilimo bora kutambua na kuthamini mchango mkubwa wa wadau wa kilimo kwa kutekeleza kwa vitendo teknolojia zote zinazofundishwa na wadau ili kuzalisha malighafi zitakazotumika na viwanda vilivyopo na vitakavyoongezeka.
Aidha niwajuze kuwa ili muweze kunufaika na uwezeshaji wa kupata mitaji ambayo ndiyo changamoto kubwa mnatakiwa kujiunga na kuimarisha vikundi na vyama vya ushirika vikiwemo vikundi vya uzalishaji, vyama vya ushirika vya mazao, na vyama vya ushirika vya kuweka na kukopa ambavyo vinaweza kuwa mkombozi kwenu kwa katoa mitaji na elimu ya ujasiriamali ambayo itasaidia kuongeza kipato na kujikomboa kiuchumi.
Sambamba na hayo amewapongeza viongozi wa wilaya katika kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji na kusma kuwa migogoro hiyo kwa kiasi kukibwa inapunguza uzalishaji mazao na uchumi hivto ameusisitiza uongozi kushirikiana na kamati za amani ngazi zote kuhakikisha ufumbuzi wa kudumu unakuwepo baina ya wakulima na wafigaji ili kila mmoja ashiriki kikamilifu kwenye uzalishaji.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa