Rai imetolewa kwa Waheshimiwa madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kuwa wasimamizi wazuri na kuepusha migogoro katika maeneo yao kwa kuhakikisha kanuni, taratibu na sheria zinafuatwa.
Rai hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Idara Utafiti, Ushauri na Mafunzo ya Muda Mfupi toka Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo Dkt. Muhsin Danga wakati wa kufunga mafunzo ya kuwajengea uwezo madiwani yaliyofanyika katika kwa siku tatu katika kata ya Mikumi ambapo amewataka madiwani hao kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuifanya Wilaya na halmashauri kiujumla kusonga mbele.
Katika mafunzo hayo madiwani hao wamejifunza mada mbalimbali ikiwemo sheria ya maadili ya viongozi wa Umma, Elimu ya rishwa, Historia na uhalali wa Serikali za Mitaa, Wajibu na majukumu ya diwani, Uendeshaji wa vikao na mikutano, Usimamizi wa watumishi, Usimamizi wa mapato na manunuzi, Uongozi na utawala pamoja na suala zima la mfumo wa fursa na vikwazo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mh. Wilfred Sumari amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji kwa mafunzo hayo na kusema kuwa mafunzo hayo yamewaongezea uwezo na kwamba wameona kuthaminiwa mchango wao kwani mafunzo hayo lilikuwa ni hitaji la madiwani ambapo amewataka madiwani hao kuboresha utendaji wao na kufanya kazi kama timu kwa kushirikiana na watendaji katika maeneo yao ili kuijenga nyumba moja ambayo ni Kilosa huku akitaka kuwepo kwa mpango wa ziara ya mafunzo kwa madiwani ili waweze kujifunza zaidi.
Naye Makamu Mwenyekiti Mh. Hassan Mkopi pamoja na Mwenyekiti wa mafunzo hayo Mh. Douglas Mwigumila wameshukuru kwa mafunzo hayo kwani wanaamini yamewapa maarifa katika utendaji wao na shughuli za Serikali kwa kuleta maendeleo kwenye maeneo yao na kwamba kwasasa wana ari mpya ya kutekeleza majukumu yao kwa kuimarika zaidi kiutendaji huku wakiomba mafunzo hayo kuwa endelevu kwa maslahi ya Halmashauri.
Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Mkuu wa Divisheni ya Utumishi Bi. Fauzia Nombo amewashukuru madiwani hao kwa ushirikiano waliouonyesha katika siku zote za mafunzo na kwamba anaamini kupitia elimu waliyopata watakuwa msaada mkubwa katika maeneo yao hususani katika kupunguza migogoro na malalamiko huku akiahidi kutoa ushirikiano katika kuhakikisha changamoto mbalimbali zinatatuliwa husuasani katika suala zima la kiutumishi.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa