Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa wameonyesha kuridhishwa na juhudi za dhati ambazo zimekuwa zikionyeshwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale kwa namna ambavyo amekuwa bega kwa bega kwa kushirikiana na madiwani pamoja na timu nzima ya menejimenti katika kuhakikisha rasilimali za Halmashauri zinatumika kadri ipasavyo na kuleta tija kwa wananchi.
Hayo yamebainishwa Juni 8 mwaka huu na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mh Hassan Mkopi alipokuwa akifungua baraza la madiwani na kusema kuwa kwa nyakati tofauti tofauti Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imekuwa na wakurugenzi mbalimbali lakini kupitia Mkurugenzi Mwambambale wanayo mambo ya kujivunia katika usimamizi wa miradi mbalimbali ambapo rasilimali zimekuwa zikitumika vizuri na kuleta tija katika miradi ya maendeleo inayoendelea maeneo mbalimbali na kuleta tija kwa wananchi.
Mkopi amesema kuwa kwa kutambua mchango wa Mkurugenzi huyo waheshimiwa madiwani waliazimia kumtunuku cheti cha pongezi ikiwa ni sehemu na ishara ya kutambua mchango wake kwa Wilaya ya Kilosa lakini pia ametumia fursa hiyo kumshukuru Mheshimiwa Rais wa awamu ya tano kwa namna ambavyo amekuwa akiitazama Wilaya ya Kilosa ambapo kwa nyakati tofauti tofauti amekuwa akitoa fedha za serikali ambazo zimekuwa msaada mkubwa katika kuendesha miradi mbalimbali katika sekta ya afya, elimu, maji, kilimo na sekta nyinginezo.
Akionyesha shukrani zake baada ya kupokea cheti cha pongezi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilossa Asajile Lucas Mwambambale amesema anawashukuru madiwani hao kwani utendaji wake wa kazi umechangiwa kwa kiasi kikubwa na madiwani ambao ndio wenye dhamana na Halmashauri na kwamba kama Halmashauri ilijiwekea malengo ambayo yamefanyiwa kazi na kupelekea Halmashauri kufika mahali illipofika.
Mwambambale amesema kama Mkurugenzi na timu ya menejimenti wamekuwa wakipata ushirikiano mkubwa kutoka kwa madiwani ambao wamekuwa chachu ya kufanya vizuri kwa kuhakikisha miradi yote iliyoko katika kata zao inasimamiwa na kufanyika katika ubora stahiki jambo lililosaidia Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kuwa mfano wa kuigwa ama chuo cha kujifunza kwa wilaya nyingine ambapo asilimia kubwa ya miradi hiyo imekuwa ikifanyika kwa ubora na thamani stahiki
Pamoja na hayo Mwambambale amewatia moyo madiwani hao na kusema kuwa ni maombi yake kuona madiwani hao wakirejea tena madarakani kwa kipindi kingine ili waweze kuliendeleza mbele gurudumu la maendeleo huku akiahidi kuendelea kufanya kazi zake kwa juhudi kwa kuhakikisha usalama wa rasilimali hususani fedha hadi hapo madiwani watakaporejea tena madarakani na kwamba kasi ya miradi ya maendeleo itaendelea kama kawaida na kwamba kazi zitaendelea kufanyika kwa uadilifu mkubwa kwa kuweka alama za maendeleo katika Wilaya ya Kilosa.
Akibainisha baadhi ya alama zilizowekwa kwa ushirikiano wa madiwani hao amesema kupitia fedha kutoka Serikalini na za mapato ya ndani ya Halmashauri imeweza kuweka alama mbalimbali za maendeleo ikiwemo kutekeleza maagizo ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa jengo la upasuaji Magubike ambalo limekamilika na alama nyinginezo ni ujenzi wa wodi mbili za wanawake na wanaume kituo cha afya Mikumi, ujenzi wa kituo cha afya Malolo, ujenzi wa vyumba vya madarasa shule ya msingi Msowero yamekamilika, ujenzi wa kituo cha afya na miundombinu ya umwagiliaji pamoja na ghala katika kata ya Mvumi na miradi mingineyo ambayo inaendelea ikiwemo ujenzi wa maabara katika shule za sekondari.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa