Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe Jerry William Silaa ametoa agizo kwa Makampuni ya Mawasiliano ya Simu Nchini kukamilisha ujenzi wa Minara ya mawasiliano758 inayoendelea kujengwa nchini kote ifikapo Mei 12, 2025.
Mhe Silaa ametoa agizo hilo Mei 14, 2025 wakati alipokuwa katika Ziara ya kikazi ya siku moja ya kukagua ujenzi wa Mnara wa Mawasiliano uliopo katika kijiji cha Idete, Kata ya Chanzuru Wilayani Kilosa.
Amesema kuwa kupitia Mradi huo wa ujenzi wa Minara 758, watanzania zaidi ya milioni 8 kutoka Mikoa tofauti tofauti watafikiwa na kunufaika na Mradi huo huku Mkoa wa Morogoro pekee ukiwa na jumla ya Minara 69 na kwamba mpaka sasa tayari Minara 24 imekwisha washwa.
Mhe Silaa amesema kuwa Mnara wa Idete ni miongoni mwa Minara hiyo 758 na unajengwa na kampuni ya Airtel Tanzania baada ya kupata ruzuku kutoka Serikalini ambapo unatarajiwa kukamilika tarehe 1 April mwaka huu na kwamba huduma zinazotarajiwa kutolewa ni 2G , 3G, pamoja na 4G hivyo wakazi wa Kijiji hicho na vijiji jirani wanatarajiwa kupata huduma hizo pindi tu Mnara huo utakapokamilika na kuwashwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe Shaka Hamdu Shaka ametoa shukrani zake kwa Waziri huyo wa Mawasiliano kwa kutembelea Wilayani Kilosa na kusema kuwa amekuwa Waziri wa kwanza kufanya Ziara katika Kijiji hicho,sambamba na hayo amesema kuwa Ujenzi wa Mnara huo umetoa fursa ya ajira kwa Vijana wa Kijiji hicho jambo ambalo litawasaidia kujikwamua kiuchumi.
Aidha amewataka Wakazi wa Kijiji hicho kuendelea kuulinda Mradi huo na Miradi mingine ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe Rais Daktari Samia Suluhu Hassan ili iweze kuhudumia kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) Mhandisi Peter Mwasyalanda amesema kuwa Wilaya ya Kilosa ina ujenzi wa Minara 18 kati ya hiyo Minara 9 tayari imeshakamilika na kuanza kutumika huku Mnara huo wa Idete unatarajiwa kukamilika aprili 1 mwaka huu.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa