Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka wawekezaji kuwekeza katika kujenga Hoteli za kisasa kwa wingi zitakazotumiwa na wageni pamoja na watalii watakaojitokeza nje na ndani ya nchi kufanya utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.
Mhe.Rais ameyasema hayo 4 Agosti, 2024 wakati akizungumza na wananchi wa Mji wa Mikumi ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake Wilayani Kilosa na kuongeza kuwa kupitia Filamu ya Royal Tour na uwepo wa Reli ya kisasa (SGR) imeongeza watalii wengi katika Hifadhi yaTaifa ya Mikumi kutoka wageni 54,021 mwaka 2019/2020 hadi kufikia wageni 138,844 mwaka 2023/2024.
Aidha Rais Samia amesema kuwa Filamu hiyo ya Utalii imekuza utalii nchini na kwa sasa serikali inawekeza kwenye miundombinu ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa watalii na kuwasisitizia wawekezaji kujenga hoteli za kisasa zitakazoweza kukidhi mahitaji ya watalii.
Kwa upande mwingine amesema kuwa Serikali ina lengo la kuunganisha reli iliyopo, reli yaTazara na reli ya SGR ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji wa bidhaa na watu ili kuleta maendeleo nchini.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa