Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imefanikiwa kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka asilimia 94 mpaka kufikia asilimia 98.91 kwa mwaka fedha uliopita wa 2022/2023, makusanyo hayo yatasaidia katika shughuli mbalimbali za Maendeleo katika wilaya hiyo.
Hayo yamesemwa 31 Agosti, 2023 na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmasahuri ya Wilaya ya Kilosa Ndg Kisena Mabuba katika Mkutano wa kawaida wa Baraza la madiwani uliofanyika katika ukumbi wa FDC Ilonga.
Mabuba amesema kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mkubwa uliofanyika baina ya wahe. Wabunge, Madiwani, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Watendaji wa halmashauri ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kila mmoja anatimiza majukumu yake.
Ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka miwili Halmashauri imeweza kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kujenga shule za Awali, Msingi na Sekondari mpya ili kupunguza mrundikano wa wanafunzi na pia kuwafikia wanafunzi wanaotembea umbali mrefu kufika shuleni sambamba na vituo vya afya katika kata mbalimbali wilayani hapo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kilosa Mhe. Wilfred Sumari amesema kuwa maendeleo ya wilaya hiyo yametokana na usimamizi mathubutu wa Mkurugenzi mtendaji na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa kwa kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati unaotakiwa.
Aidha akizungumzia upande wa utunzaji wa mazingira Mhe Mwenyekiti amesema Halmashauri imejiwekea Mkakati wa kuhakikisha mazingira na vyanzo vya maji vinakuwa salama kwa kusimamia sheria za mazingira ili kutunza vyanzo hivyo.
Awali katika Mkutano huo Diwani wa kata ya Magubike Mhe. Abuu Msofe aliapishwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mh. Agnes Ringo baada ya kushinda uchaguzi mdogo uliofanyika Julai 13,2023 baada ya diwani aliyekuwa akiongoza kata hiyo kufariki dunia .
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa