Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale ametoa rai kwa wakuu wa vyuo, wakuu wa shule pamoja na idara ya Elimu Sekondari kiujumla kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa corona kufuatia agizo la Serikali kuwataka wanafunzi wote wa vyuo na kidato cha sita kuanza masomo yao Julai mosi mwaka huu huku akitaka kuzingatiwa kwa maelekezo ya Serikali dhidi ya janga la corona.
Mwambambale ametoa rai hiyo Juni mosi mwaka huu katika mafunzo kwa wakuu wa vyuo na shule kuhusu hatua stahiki za kuchukua kipindi ambacho vyuo na shule zinapofunguliwa ambapo amesema kuwa licha ya athari mbalimbali zilizojitokeza kutokana na janga la corona na kwamba anamshukuru Mheshimiwa Rais wa awamu ya tano ambaye ugonjwa wa korona ulipoingia nchini hakutaka nchi isimame kwa kusimamisha shuguuli za kila siku badala yake alisisitiza shughuli za uzalishaji na maendeleo kuendelea kama kawaida huku akisisitiza kuzingatiwa kwa tahadhari ili kuwa salama.
Aidha amepongeza mwitikio ulioonyeshwa na wakuu wa shule na vyuo kwa juhudi na maandalizi yaliyofanyika ndani ya muda mfupi kwa ajili ya kuwapokea wananfunzi ambao wameanza rasmi masomo yao Juni mosi mwaka huu ambapo ametaka kuendelea kufanyika juhudi za makusudi kwa kuhakikisha maelekezo yote ya Serikali yanazingatiwa ikiwemo kuwasaidia wanafunzi wanaowasili na kuwepo vyuoni na mashuleni kuzingatia kanuni na taratibu zote kwani wanafunzi wanapokelewa na kurejea mashuleni kungali kukiwa na ugonjwa wa corona.
Mwambambale amesema mafunzo hayo yanalenga kutambua kwa haraka viashiria vya maambukizi ya corona lakini pia kuchukua hatua za haraka pindi vinapobainika viashiria kwani kama wasimamizi wanao wajibu kuyafanyia kazi mafunzo haya na kulinda maisha ya wanafunzi kwa kuwafanya wawe salama wawapo shuleni kwa kuzingatia kikamilifu misingi ya kuepuka corona kwao binafsi na kwa wanafunzi ikiwemo kuzingatia ukaaji wa mita moja toka mtu mmoja kwenda mwingine, unawaji mikono mara kwa mara, matumizi ya vitakasa mikono, uvaaji wa barakoa lakini pia amesema endapo kutakuwa na viashiria vya maambulizi ya corona mawasiliano yafanyike kwa haraka ili kuchukua hatua stahiki huku akisisitiza kutolewa elimu kwa wanafunzi ili wasisite kutoa taarifa kwa ajili ya kupata msaada mapema na wa karibu.
Naye Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari Wilaya Bi. Paula Nkane amewataka washiriki hao kuhakikisha wanayafanyia kazi mafunzo hayo ikiwemo kuendelea kutoa elimu kwa walimu wenzao sambamba na kwa wanafunzi mara kwa mara kwa kuhakikisha maelekezo yotre ya Serikali na ya wataalam wa afya yanafuatwa kikamilifu pamoja na kutoa taarifa kwa haraka pindi wanapokutana na changamoto za aina yoyote.
Kwa upande wa wataalam wa afya toka hospitali ya wilaya ya kilosa afisa afya John Nyange, mtaalam wa maabara Lucas Kasinje na Dkt Anna Malele ambapo kwa niaba ya wenzake Dkt. Malele amesema kuwa virusi vya corona huathiri zaidi njia ya mapafu na kwamba zipo dalili mbalimbali kama vile kukohoa, homa, kupumua kwa shida, maumivu ya kichwa mwili kuishiwa nguvu na kwamba asilimia kubwa ya watoto na wazee ndio wahanga wakubwa wa corona smbamba na wale wenye magonjwa ya kudumu ya presha na kisukari.
Aidh Dkt. Malele amesema si kila mgonjwa anayepumua kwa shida au mwenye dalili zilizotajwa kuwa ana corona hivyo amewataka washiriki hao pindi wanapobaini viashiria vya corona kutoa taarifa kwa wataalam wa afya ili kupata msaada wa karibu kwa ajili ya wahisiwa ili vipimo viweze kufanyika kwa haraka ambapo ametaka kila shule/ chuo kuwa na chumba maalum kwa ajili ya wale wahisiwa kabla ya kuchukuliwa hatua zaidi za kitabibu na wataalam wa afya.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa