Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imechukua hatua ya kuboresha usimamizi na ufatiliaji wa marejesho ya mikopo inayotolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu kwa kununua gari aina ya Land Cruiser Hard Top yenye thamani ya shilingi Milioni 226 fedha kupitia marejesho ya mikopo ya asilimia 10%.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha ufuatiliaji wa karibu na ufanisi katika urejeshaji wa mikopo hiyo, ambayo ni sehemu ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri yanayotengwa kwa ajili ya makundi maalum.
Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Mkuu wa Divisheni ya Mipango na Uratibu, Wapa Mpwehwe, amesema kuwa kwa mujibu wa sheria ya mikopo, asilimia 15 ya marejesho ya mikopo hutumika kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliaji na kwamba badala ya kutumia fedha hizo kwa posho, halmashauri imeamua kununua gari hilo ili kuongeza ufanisi katika shughuli za usimamizi wa mikopo.
Mpwehwe ametoa wito kwa watendaji wa halmashauri kuhakikisha gari hilo linatunzwa vizuri na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa,huku akiwataka wanufaika wa mikopo hiyo kurejesha kwa wakati ili fedha hizo ziweze kuwasaidia watu wengine katika jamii.
Halmashauri ya Kilosa imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali ya kuhakikisha mikopo inayotolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu inarejeshwa kwa wakati na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kwamba hatua ya kununua gari kwa ajili ya usimamizi wa mikopo ni sehemu ya mikakati hiyo ya kuhakikisha ufanisi na uwajibikaji katika utoaji na urejeshaji wa mikopo.
Kwa hatua hyo, Halmashauri ya Kilosa inaonyesha dhamira ya dhati ya kuimarisha mifumo ya usimamizi wa mikopo na kuhakikisha kuwa rasilimali zinazotolewa zinatumika kwa manufaa ya jamii nzima, hasa makundi maalum yanayolengwa na mikopo hiyo.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa