Machi 20 mwaka huu katika Maadhimisho ya Siku ya Afya ya Kinywa na Meno Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi amewataka matabibu wa afya ya kinywa na meno kupanua afua za kitabibu kulingana na miongozo mbalimbali ya huduma za afya ya kinywa na meno ikiwemo kuwa na ratiba za kutembelea shule za msingi na sekondari kwa lengo la kutoa elimu, ushauri, uchunguzi na matibabu kwa wale watakaobainishwa kuwa na matatizo.
Mgoyi amesema kuwa pamoja na kupanua afua hizo wanatakiwa kuwawezesha kwa kuwajengea uwezo watumishi katika vituo vya afya na wale wanaotoa huduma za afya majumbani pamoja na kuwezesha utoaji wa huduma ya mkoba ya afya ya kinywa na meno ili kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wananchi walio mbali na vituo vya kutolea huduma za kinywa na meno.
Akiongea na wananchi waliofika kufanya uchunguzi wa afya ya kinywa na meno Mgoyi amesema kuwa serikali inatambua upungufu mkubwa wa watoa huduma wakiwemo madaktari wa kinywa na meno ambapo Serikali ya awamu ya Tano inaendelea kupambana na kutatua changamoto za watoa huduma za afya ya kinywa na meno lengo ikiwa kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo.
Aidha amewataka wananchi kufahamu kuwa uchunguzi wa afya ya kinywa na meno ni muhimu hivyo ni vyema jamii ikahamasi ka na kuwa na hulka ya kwenda hospitali kufanya uchunguzi wa kinywa na meno ili kujihakikishia usalama wa kinywa na meno.
Naye daktari wa Afya ya Kinywa na Meno Mkoa wa Morogoro Dkt Samson Tarimo amesema kuwa kaulimbiu katika maadhimisho hayo ni Sema aaah, chukua hatua zinazingatia katika Afya ya Kinywa na Meno na kwamba lengo la maadhimisho hayo ni kujenga uelewa na kutoa matibabu kwa matatizo ya afya na kinywa na kwamba katika maadhimisho hayo wamefanikiwa kutoa huduma katika shule za msingi Kilosa Town, Mazinyugu na Kichangani sambamba na kwa wananchi ambapo matatizo yaliyobainika ni kuoza na kutoka kwa meno, fizi na mpangilio mbaya wa meno.
Sambamba na hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Lucas Mwambambale amewataka matabibu wa afya kuwa na mpango kazi wa namna ya kutoa huduma kupitia fursa za mikutano mbalimbali ya vijiji ili kutoa elimu na huduma ya afya ya kinywa na meno lakini pia amewashukuru wadau mbalimbali na hasa madaktari waliotoa huduma za afya ya kinywa na meno na amewataka kuendelea kutoa huduma kwa kuweka mbele zaidi taaluma yao.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa