Kupitia ushirikiano ambao umekuwa ukionyeshwa na viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Kilosa umekuwa chachu kubwa ya kupunguza migogoro mbalimbali ambayo ilikuwa ikiikabili katika maeneo mbalimbali ikiwemo migogoro ya ardhi, migogoro ya wakulima na wafugaji iliyokuwa ikileta athari mbalimbali katika maisha ikiwemo vifo.
Hayo yamebainishwa Septemba 17 mwaka huu na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi wakati akifungua kikao maalum kilichokuwa kikijadili mpango wa ujenzi wa shule ya sekondari ya bweni kwa ajili ya watoto wa kike akiwa kama mgeni rasmi ambapo amesema kuwa awali kulikuwa na kesi 1580 zilizotokana na migogoro ardhi na kuleta athari mbalimbali ikiwemo kutokuwepo kwa amani, kutovuna mazao kwa wakati kwa wakulima kuvuna mazao yasiyokomaa na kusababisha mazao kuwa na sumu kuvu ambapo kwa sasa migororo hiyo imepungua kwa kiasi kikubwa na kufikia kesi 25 hadi kufikia mwezi Machi jambo ambalo ni la kujivunia na sehemu ya mafanikio.
Mgoyi amesema licha ya mafanikio hayo bado wanaendelea kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo kukabiliana na baadhi ya wafugaji wanaoendelea kuwaonea wakulima lakini pia wakulima au madalali wanaoendelea kujinufaisha kwa njia za ulaghai kwa kudai fidia na kujipatia kipato kinyume cha sheria huku akisema upande wa migogoro ya ardhi Serikali ya awamu ya tano imeendelea kufuta mashamba ambayo yamekuwa hayaendelezwi.
Aidha amesema Wilaya ya kilosa inahitaji mwarobaini wa kutibu migogoro ya ardhi ambapo wilaya inahitaji kuwa na mpango bora wa matumizi ya ardhi mpango ambao anaamini utakuwa ndio suluhisho la migogoro ya ardhi na kwamba anaamini wananchi wataichagua tena Serikali ya awamu ya tano chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli ili itakaporudi madarakani kwa kipindi kingine iweze kukamilisha deni hilo kwa wananchi.
Pamoja na hayo amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale kwa juhudi alizozionyesha hususani katika kusimamia na kuhakikisha fedha za ndani zinazokusanywa na Halmashauri kwa asilimia kubwa zinatumika kufanya shughuli za maendeleo ikiwemo ujenzi wa vituo mbalimbali vya afya, ujenzi wa mabweni shule ya sekondari Kimamba, mradi wa maji Ruaha, ujenzi wa jengo la upasuaji Magubike, ujenzi wa madarasa sambamba na ujenzi wa vibanda eneo feri hivyo ni mafaniko makubwa kuona fedha za umma zinatumika ipasavyo.
Pamoja na hayo amesisitiza licha ya kufanikisha mambo mbalimbali lipo jukumu kwa viongozi kwa pamoja kujenga msingi mzuri kwa watoto kwa kuwapatia elimu iliyo bora kwa kuwa na rasilimali watu na majengo pamoja na kuwa na usimamizi mzuri kwa kuhakikisha watoto wanapata elimu bora yenye kuleta tija kwa kuwa na matokeo mazuri katika sekta ya elimu ambapo kwa sasa Wilayaya Kilosa imekuwa ikipanda na kuwa na matokeo mazuri.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa