Novemba 4,2022 Naibu Waziri wa Kilimo, Mh.Antony Mavunde amezindua rasmi ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika mashamba ya uzalishaji wa mbegu yaliyo chini ya Wakala Wa Mbegu za Kilimo(ASA) mradi ambao utakaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 18 ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa Serikali kuzalisha mbegu bora kwa kipindi cha kiangazi ili kuondokana na changamoto ya uhaba wa mbegu na kuongeza upatikanaji wake unapofika msimu wa kilimoa mabpo uzinduzi huo umefanyika katika shamba la msimba katika kata ya Chanzuru.
‘’Dhamira ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuondoa changamoto zinazomkabili mkulima ikiwemo upatikanaji hafifu wa mbegu bora msimu wa kilimo, kwa kuona hili Serikali imeongeza bajeti katika kilimo ili kuweka mbiundombinu ya umwagiliaji kwenye mashamba ya mbegu ambayo itapelekea mbegu bora kuzalishwa kabla ya kuanza kwa msimu wa kilimo, ambapo visima vitano virefu vya maji vilivyochimbwa hapa vitasaidia kuzalisha maji yatakayohifadhiwa katika bwawa lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni 45’’. Amesema Mh. Mavunde
‘’Huu ni mwanzo wa mabadiliko makubwa yanayokuja katika uzalishaji wa mbegu bora hapa nchini ili tufikie lengo la uzalishaji wa mbegu wa kutosheleza mahitaji ya nchi na kupata ziada ya kuuza nje ya nchi. Hivyo ASA hakikisheni mnaishirikisha sekta binafsi katika uzalishaji wa mbegu bora kwakuwa ili tuweze kufikia malengo lazima tuunganishe nguvu kwa pamoja baina ya serikali na sekta binafsi na kamwe hampaswi kuwa washindani bali mtegemeane kwa manufaa ya nchi’’.
Aidha Mh. Mavunde amemuagiza Mtendaji Mkuu wa ASA, Dkt. Sophia Killenga-Kashenge kuhakikisha mashamba yote ya ASA yanalimwa na kuongeza uzalishaji wa mbegu, badala ya kuyaacha kama mapori kama ilivyo sasa sambamba na kuwekewa uzio ili kuyalinda na uvamizi kutoka kwa watu mbalimbali ambao wanayaona kama hayatumiki.
Sambamba na hayo amewaomba wadau wote tushirikiane kwa pamoja katika kutekeleza mipango ya serikali kukuza sekta ya kilimo kupitia utekelezaji wa Vipaumbele vya Wizara ya Kilimo kupitia Ajenda 10/30 ambavyo ni kuimarisha utafiti, kuongeza uzalishaji wa mbegu, kuimarisha huduma za ugani, umwagiliaji na kuwezesha upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa mazao ya wakulima.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Alhaj Majid Mwanga ameishukuru Serikali kwa kupeleka mradi huo mkubwa Kilosa na kusisitiza kuwa wataendelea kushirikiana na ASA bega kwa bega ili mradi huo uweze kuleta tija kwa wananchi wa Kilosa na Tanzania kwa ujumla.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa