Mbunge wa Jimbo la Mikumi, Mhe. Denis Londo, amekabidhi gari la kubebea wagonjwa mahututi (ambulance) katika Kituo cha Afya cha Ulaya kilichopo Tarafa ya Ulaya wilayani Kilosa, akitoa shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta msaada huu muhimu kwa wananchi wa jimbo hilo.
Katika hafla hiyo, Mhe. Londo amesema kuwa gari hilo litakuwa ni msaada mkubwa katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi, hasa wakati wa dharura ambapo usafiri wa haraka ni muhimu na kwamba wananchi wa Jimbo la Mikumi wanahitaji huduma bora za afya, na kuleta gari la kubebea wagonjwa ni moja ya jitihada za serikali kuhakikisha kuwa huduma za afya zinawafikia wananchi kwa wakati.
"Gari hili ni mkombozi kwa wananchi wa Ulaya na maeneo mengine jirani na tunamshukuru Rais Samia kwa kutujali na kutuletea huduma hii, ni muhimu sana kutunza gari hii kama mboni ya jicho ili iweze kutumika kwa muda mrefu na kuendelea kutoa huduma kwa wananchi ambapo linakwenda kutatua changamoto kubwa ya usafiri kwa wagonjwa wa dharura” alisema Mhe Londo.
Katika hatua nyingine wakati akizungumza na wananchi, Mhe. Londo amewataka kutosikiliza maneno ya watu wanaoharibu sifa ya serikali huku akiwakumbusha kuwa serikali ya Rais Samia inatekeleza miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi, akitaja ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mikumi hadi Kilosa na ujenzi wa karavati kubwa la Nyali kama mifano ya juhudi za serikali kuboresha miundombinu ya wilaya hiyo.
"Serikali ya Rais Samia inatekeleza miradi ya maendeleo kwa ufanisi ambapo Ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mikumi hadi Kilosa uko mbioni kuanza, na pia ujenzi wa karavati kubwa la Nyali ambao utawezesha usafiri wa haraka zaidi," alisema Mhe. Londo.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi Sara Ally ukomelangani na Mussa Ndekelo wamemshukuru mbunge kwa kuwaletea maendeleo katika jimbo lao ambapo walikua na changamoto ya gari kwa muda mrefu na wengine walikua wanafia na kujifungulia njiani pamoja na kutumia gharama kubwa za kukodi usafiri hivyo wanaipongeza serikali kwa kuwapatia usafiri huo wa haraka.
Awali akizungumza Mkuu wa Divisheni ya Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe wilaya ya Kilosa Dkt Seleman Kasugulu ameishukuru serikali kwa kutoa gari la kubebea wagonjwa mahututi, akisema kuwa itakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa maeneo ya vijijini ambapo gari hilo litasaidia kwa kiasi kikubwa usafiri wa wagonjwa kutoka vijijini hadi kwenye kituo cha afya na hospitali, jambo ambalo lilikuwa ni changamoto kubwa kwa muda mrefu.
DMO Kasugulu amesema kuwa kwa muda mrefu, wagonjwa walikuwa wanalazimika kusubiri gari kutoka hospitali kuu ya wilaya ya Kilosa, halo iliyosababisha kuchelewa kwa huduma za afya na kusababisha vifo hivyo kupatikana kwake utakuwa msaada katika kupunguza muda wa kusafiri na kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma za afya kwa wakati huku akisisitiza umuhimu wa kutunza gari hilo kwa ustawi wa jamii.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa