Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kilosa Mhe. Wilfred Sumari amewataka wakazi wa Kilosa kuchangia maoni na mapendekezo yao kwenye kuandaa Dira ya Taifa ya maendeleo ya mwaka 2050 ili kuijenga Tanzania waitakayo ya mwaka 2050.
Wito huo ameutoa katika kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya kilichofanyika Julai 26, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa FDC Ilonga kilichokutanisha makundi mbalimbali ya wananchi, wataalamu na wadau wa maendeleo kwa lengo la kutoa maoni yao kuhusu maandalizi ya dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Mhe. Sumari amesema kuwa kila mwanachi ana haki ya kutoa maoni yake na kuongeza kuwa maoni hayo yatachukuliwa na kufikishwa sehemu husika na yatatumika katika kuiandaa dira hiyo.
Akifafanua historia ya Tanzania pamoja na vipindi vya maendeleo iliyopitia Tanzania kabla, wakati na baada ya ukoloni, mbunge wa Kilosa Mhe. Prof. Palamagamba kabudi amewataka wanakilosa kuchangia maoni yao kwenye Dira hii kwa kuzingatia misingi muhimu kama vile kudumisha utamaduni, kuimarisha uchumi wa viwanda, teknolojia na kuboresha mifumo ya Elimu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Ndg. Michael Gwimile amewataka washiriki wa kikao hicho kuwa mabalozi kwa wenzao ambao hawakushiriki kikao hicho kwa kuwaelekeza namna ya kuchangia maoni yao kwa njia ya simu za mikononi.
Naye Mkuu wa Divisheni ya Mipango na Uratibu wa Halmashauri ya wilaya ya Kilosa Wapa Mpwehwe amefafanua namna ya kutoa maoni kwenye maandalizi ya dira hii kwa njia ya simu za mkononi kwa kutumia menyu ya *152*00# au kwa njia ya intaneti na kuongeza kuwa kila mwananchi mwenye umri kuanzia miaka 15 na kuendelea anaruhusiwa kutoa maoni yake.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa