Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi Mei 24, 2018 amewahimiza wanamichezo wote wanaoshiriki katika mashindano ya UMISSETA ngazi ya Halmashauri kutambua kuwa michezo ni sehemu ya kufanya maandalizi na kujionyesha kwa ajili ya ajira kwani wachezaji wakubwa nchini kama kina Thomas Ulimwengu wanapata pesa nyingi kupitia mpira wa miguu jambo linalothibitisha kuwa michezo ni ajira.
Mgoi ambaye alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mashindano hayo ngazi ya Halmashauri yenye kauli mbiu ’’Michezo Sanaa na Taaluma ni msingi wa wanafunzi katika maendeleo ya Taifa letu’’ amewataka wanamichezo waliochaguliwa kuunda timu ya wilaya na kuwakilisha vyema katika mashindano, hivyo wanapaswa kujituma, kujenga moyo wa ushindani na kuweka nidhamu mbele.
Aidha ametoa rai kwa walimu kuwa kioo cha jamii pamoja na kutumia sheria na taratibu za kazi kwa maslahi ya taifa jambo litakalosaidia kutokuwa chanzo cha kuwakatisha masomo wanafunzi kwa sababu zozote zile bali kusambaza ujumbe wa malezi bora kwa wanafunzi wote.
Akisoma risala kwa mgeni rasmi Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari Paula Nkane amesema mashindano hayo ya siku nne yanayofanyika katika viwanja vya Shule Sekondari Mazinyungu yanashirikisha clasta za Kilosa, Kimamba. Mikumi, Zombo na Dumila ambapo zitacheza michezo mbalimbali ikiwemo riadha, mpira wa wavu, mpira wa kikapu, soka, netbali na fani za ndani na kupitia michezo hiyo wanafunzi wataweza kuongeza uelewa darasani na kuongeza taaluma kwani michezo huimarisha afya ya akili na mwili.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa