Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka amewata wanufaika wa mikopo ya asilimia kumi ya mapato ya ndani kutumia mikopo hiyo kwa ajili ya kutekeleza shughuli mbalimbali za miradi wanayoifanya ili kujiongezea kipato kwa mtu mmoja mmoja na kuinua uchumi wa Taifa.
Mhe. Shaka ameyasema hayo tarehe 21Janauari, 2025 wakati wa uzinduzi wa utaoaji wa mikopo ya 10% ambapo katika hafla hiyo Mhe. Shaka amekabidhi hundi ya mfano yenye kiasi cha shilingi Milioni 547,000,000 na kusema kuwa fedha hizo zimetolewa ili zikatekeleze shughuli mbalimbali zinazofanywa na vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Mhe. Shaka ameongeza kuwa mikopo hiyo imetolewa kwa vikundi hivyo ili vikazalishe na kurejesha fedha hizo kwa wakati ili ziweze kuwanufaisha wananchi wengine.
“Mtakapo rejesha kwa wakati ndipo ambapo fedha hizo zitakwenda kuwanufaisha watu wengi zaidi na wanufaika wataongezeka siku hadi siku”. Alisema Mhe Shaka
Aidha Mhe Shaka ametoa wito kwa wakazi wa Kilosa kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kushamirisha maendeleo na kutunza amani ya nchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Ndg. Michael J. Gwimile amesema lengo la mikopo hiyo ni kusaidia wananchi waweze kufanya shughuli za kiuchumi. Vilevile amewataka wanufaika wa mikopo hiyo kuendeleza tabia nzuri walizokuwa wakizionesha kabla ya kupokea mikopo hiyo.
“Mkawe mfano kwenye kusimamia miradi yenu, kama lengo ambalo mmeliandika kwenye mradi wakati wa kuomba mkopo mkasimame kwenye lengo hilo”. Alisema Gwimile
Pia Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Ndg. Alto Mbikiye amesema jumla ya fedha kiasi cha shilingi Milioni 547zimetolewa kwa vikundi 60 ambapo fedha hizo zimegawanyika katika makundi matatu , 4%kwa wanawake, 4% kwa vijana na 2% kwa watu wenye ulemavu.
Naye mmoja wa wanufaika wa mikopo hiyo Ndg.Iman Mtewele ameishukuru serikali kwa kuwaamini na kuwapatia mikopo hiyo ambayo itakwenda kuwasaidia kutimiza malengo waliojiwekea ili kuimarisha uchumi wao.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa