Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kwebe S. Kebwe amewataka wataalam wilayani Kilosa hasa katika sekta ya ujenzi kusimamia kikamilifu ujenzi wa miradi mbalimbali inayoendelea lengo ikiwa kupata majengo ama miundombinu iliyo bora.
Kebwe amesema hayo katika ziara ya siku mbili wilayani Kilosa ambapo amesema ni vema wataalam wakasimamia badala ya kuwaachia mafundi jambo ambalo linaweza kusababisha miradi kutokamilika katika kiwango kinachostahili.
Akizungumzia upande wa ukusanyaji mapato Kebwe amesema mwaka 2019 ni mwaka wa kutafuta fedha kwani wilaya ina vyanzo vingi vya mapato hivyo anategemea kupanda kwa mapato toka 84% iliyopo sasa.
Aidha amewakumbusha wazazi na walezi kuchangaia chakula mashuleni huku akiagiza kukamatwa kwa wanaume wanaowapa wanafunzi mimba kwani tendo la kuwapa wanafunzi mimba ni kuwakatishia ndoto zao huku akisisitiza kuendelea kwa ujenzi wa madarasa kwani kupitia mfumo wa elimu bila malipo kumekuwepo na ongezeko kubwa la wanafunzi huku akitoa ahadi ya kuchangia shilingi milioni moja kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu.
Sambamba na hayo amemwagiza Injinia wa maji Mkoa kukaaa na Halmashauri ili kuweka mkakati wa kuboresha miundombinu ya maji pamoja na kuendeleza ujenzi wa zahanati katika kata ya Malolo ili huduma zianze mara moja.
Kebwe katika ziara yake ametembelea na kukagua shamba darasa la kufundishia wafugaji linalomilikiwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya Ameir Mbarak ambapo amewahamasisha wananchi kufuga kwa tija na kuachana na ufugaji wa kuhamahama kwani shamba hilo ni mfano wa kuigwa ambapo mifugo inahudumiwa kitaalam
Naye Mbunge wa Jimbo la Mikumi Mh. Joseph Haule licha ya kutoa ahadi ya kumalizia matundu ya vyoo shule ya msingi Ruaha Darajani , pia ameahidi kutoa mifuko 400 ya saruji kwa kituo cha Afya cha Malolo na Mikumi pamoja na viti na meza 60 shule ya Sekondari Mwega huku akiiomba serikali kutatua changamoto ya barabara katika kata ya Malolo sambamba na huduma ya maji.
Ziara hiyo ya Mkuu wa Mkoa ilihitimishwa kwa ugawaji wa vitambulisho kwa wajasiriamali wadogo wadogo tendo lililofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi ambapo Kebwe amesema vitambulisho hivyo ni faraja kwa wajasiliamali na kwamba vigawiwe kwa walengwa wanaostahili kwani vimetolewa na Mheshimiwa Rais wa awamu ya Tano kwa ajili ya wajasiriamali wadogo hivyo lisifanyike kisiasa.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa