Katika mwendelezo wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu, Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Ndg. Ismail Ally Ussi, amezindua rasmi Mradi wa usambazaji wa maji katika Kata ya Ulaya, Kijiji cha Ulaya Kibaoni, wilayani Kilosa.
Mradi huo unalenga kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa eneo hilo, hususan wanawake na watoto ambao wamekuwa wakikumbwa na changamoto ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji.
Akizungumza baada ya kukagua na kupokea taarifa ya mradi huo, Ndg. Ussi ameeleza kuridhishwa kwake na utekelezaji wa mradi huo wenye thamani ya shilingi milioni 177.9 na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaletea wananchi wa Kilosa Miradi ya maendeleo ambapo amesisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kumuunga mkono Mheshimiwa Rais katika juhudi zake za kuwaletea maendeleo endelevu.
Sambamba na hayo Ndg. Ussi pia ametembelea mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya cha Ulaya Mbuyuni, ambao umegharimu zaidi ya shilingi milioni 510 ambapo amekagua maendeleo ya ujenzi na kuweka jiwe la msingi, akieleza matumaini yake kuwa kituo hicho kitaboresha huduma za afya kwa wakazi wa eneo hilo na maeneo jirani.
Aidha, kiongozi huyo amepokea taarifa kuhusu hali ya malaria, UKIMWI, lishe, na uchangiaji wa damu salama katika kata hiyo na ametoa wito kwa wananchi kuzingatia lishe bora, kupima afya mara kwa mara, na kushiriki kikamilifu katika shughuli za afya ya jamii ili kuboresha ustawi wao.
Wananchi wa Kata ya Ulaya wameeleza furaha yao kwa ujio wa Mwenge wa Uhuru na Miradi hiyo ya maendeleo na kwamba upatikanaji wa maji safi na huduma bora za afya utaboresha maisha yao na kuchangia katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Mwenge wa Uhuru utaendelea na mbio zake katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Kilosa, ukikagua na kuzindua miradi ya maendeleo, kabla ya kuelekea wilaya nyingine. Kaulimbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu ni “Jitokeze kushiriki uchaguzi wa mwaka huu 2025 kwa amani na utulivu”.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa