Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imetakiwa kutekeleza na kusimamia vyema shughuli zote za miradi ya BOOST na kuhakikisha inamalizika kwa wakati na kwa kiwango kinachostahili ili kuleta tija kwa wananchi wa eneo husika.
Hayo yamesemwa 19 Septemba, 2023 na Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Mipango na Uratibu Mkoa Bw. Anza- Amen Ndossa wakati akifanya ukaguzi wa miradi ya Boost katika kata za Mtumbatu, Dumila na Msowero ambapo miradi hiyo hipo kwenye hatua ya umaliziaji.
Bw. Ndossa amesema kuwa ili kufanikisha miradi hiyo Wahandisi wanapaswa kuzingatia maelekezo wanayopewa kutoka Tamisemi na kufanya kazi kwa weledi mkubwa ikiwemo kutatua changamoto zinazojitokeza ili kukamilisha miradi hiyo kwa wakati kulingana na bajeti iliyopo,sambamba na hayo pia amepongeza hatua ya miradi ilipofikia.
Bw. Ndossa amesisitiza kuwa shule zote zinatakiwa kuboresha miundombinu ya mifumo ya maji ili wanafunzi pamoja na walimu waweze kupata maji safi na salama katika eneo la shule ambapo itasaidia kuepuka magojwa mbalimbali kama vile Kipindupindu , U.T.I na Corona lakini pia amewataka viongozi wa viijiji pamoja na kamati za shule kutunza miundombinu hiyo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashuri ya Wilaya ya Kilosa Bi. Zakhia Fandey amesema kuwa atatekeleza na kuyafanyia kazi changamoto zinazojitokeza kwenye miradi hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati na kufikia lengo lililokusudiwa na Serikali.
Timu hiyo ya ukaguzi ya miradi ya maendeleo ya sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro ikiongozwa na Katibu Tawala Msaidizi wamefanya ukaguzi wa miradi ya BOOST katika kata za Dumila, Mtumbatu na Msowero ambapo kiasi cha shilingi Bilioni 1,089,100,000 zimetolewa kupitia mradi wa BOOST kwa ajili ya ujenzi wa shule tatu.
Akitoa mchanganuo wa fedha hizo Fandey amesema Kata ya Dumila ilipokea Mil.475,300,000 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 14 vya madarasa elimu msingi, madarasa 2 elimu ya awali, jengo la utawala, matundu 24 ya vyoo na kichomea taka, Kata ya Mtumbatu ilipokea Sh. Mil 306,900,000 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 7 elimu msingi, madarasa 2 elimu ya awali, matundu ya vyoo16, jengo la utawala na kichomea taka huku Kata ya Msowero ikipokea Sh. Mil.306,900,000 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 7 vya madarasa elimu msingi, madarasa 2 elimu ya awali, jengo la utawala, matundu 16 ya vyoo na kichomea taka.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa