Waathirika wa mafuriko Wilayani Kilosa wamepatiwa msaada wa mahitaji mbalimbali kama vile chakula, mavazi, malazi na vyombo venye thamani Shilingi Milioni 50 ili waweze kujikwamua kimaisha katika kipindi hiki kigumu.
Akikabidhi msaada huo Disemba 12, 2023 mkoani hapo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima amesema baada ya kutokea kwa changamoto hiyo wadau mbalimbali kwa kushirikiana na Serikali imechanga fedha na kununua mahitaji mbalimbali ili kuwasaidia waathirika hao.
Mhe. Malima amesema kuwa wananchi 4700 wameathirika na mafuriko hayo huku nyumba 997 zikizingirwa na maji na nyumba 85 zimesombwa na maji kabisa na wananchi kukosa makazi ya kuishi.
Ameongeza kuwa mafuriko hayo yamesababisha uharibifu wa miundo mbinu mbalimbali ikiwemo madaraja manne na Barabara Pamoja na uharibifu wa mashamba ya vyakula na mali nyingine na kusabisha vifo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka ameishukuru serikali, kamati ya ulinzi na usalama za mkoa na wilaya pamoja na wadau mbalimbali kwa ushirikiano wao kwa kutoa misaada hiyo kwa wananchi walioathirika na mafuriko.
Pia Mhe. Shaka amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa kuipatia wilaya ya kilosa shilingi Bilioni 13 kwa ajili ya kuboresha miundo mbinu ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza maafa ukilinganisha na kipindi cha awali huku akibainisha kuwa waathirika hao bado wanahitaji misaada hivyo ameomba wadau mbalimbali kujitokeza kutoa msaada kwa waathirika hao.
Akizungumza kwa niaba ya wadau, Meneja wa Bank ya NMB kanda ya kati Bi. Janeth Shango kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa Bank hiyo ametoa pole kwa wananchi walioathirika Wilayani Kilosa ambapo Benki hiyo imetoa shilingi milioni 10.
Bi. Janeth amesema kuwa Benk hiyo ina utaratibu wa kutoa sehemu ya faida wanayoipata kwa wananchi hususani kwa waliopata matatizo mbalimbali ili kuungana na Serikali katika kupunguza changamoto kwa wananchi ikiwemo hili la mafuriko.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa