Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi ameutaka uongozi wa shamba la miwa la Mkulazi kutambua umuhimu wa wakulima wa nje kwenye shamba hilo kwani uwepo wa wakulima wa nje utasaidia kwa kiasi kikubwa kukua kwa shamba hilo kwani bila wakulima wa nje kiwanda hakiwezi kufanikiwa.
Mgoyi amesema kuwa wakulima wa nje ni wa muhimu licha ya changamoto mbalimbali zilizowahi kutokea kipindi cha nyuma na kwamba hawapaswi kuangalia changamoto hizo kama kikwazo bali wasonge mbele na kuchukua changamoto hizo kama fursa ya kujifunza na kusonga mbele huku ikitambua umuhimu mkubwa wa wakulima wa nje kwa kuhakikisha katika mipango yao wanawahusisha wakulima wa nje.
Awali changamoto zilizojitokeza katika kilimo hicho ni miwa kupandwa nje ya wakati, uhaba wa maji, matunzo hafifu ya mashamba , kutokuwa na uongozi thabiti wa Magole joint, elimu ndogo ya kilimo bora cha miwa ikiwemo kukosa usimamizi na kwamba kwa sasa Mkulazi inapaswa kuwatumia ipasavyo wataalam wa kilimo kwa kuhakikisha wanapata huduma stahiki ili kuondokana na umaskini ili tuweze kuelekea uchumi wa kati kwa mafanikio.
Mgoyi amesema kuwa suala la uzalishaji sukari ni la wote hivyo kila mtu aone umuhimu wa kuwa na kiwanda cha sukari, hivyo ameiagiza Halmashauri na wataalam wake kuhakikisha inawasimamia wakulima walime kwa utaratibu na usimamizi mzuri ambapo mwisho wa mwaka Halmashauri itakuwa na uwezo wa kupata zaidi ya shilingi bilioni moja kutokana na kodi kupitia kilimo cha miwa, hivyo Halmashauri , Mkulazi ambaye ndio msimamizi mkuu pamoja na wakulima kila mtu atekeleze wajibu wake ili kufikia malengo hayo na kwamba ofisi yake haitasita kumchukulia hatua yoyote atakayesababisha kutofikia malengo.
Akizungumzia suala la mkopo wa 100% amesema haliungi mkono kwani haiwezekani benki kuwakopesha 100% na kitendo hicho jambo lisilowezekana duniani na ndilo lililosababisha kufika katika changamoto zilizojitokeza kwani kuhitajika kwa mkopo huo kwa 100% kumefanya athari kwa wakulima kwa kujikuta wakisubiri mkopo badala la kujishughulisha hivyo tatizo hilo litafutiwe ufumbuzi na kwamba mkulima anayejiona hawezi ni vema akaacha kujiingiza katika kilimo hicho.
Naye Meneja wa benki ya Azania tawi la Morogoro Liberia Peter amesema kuwa licha ya changamoto zilizojitokeza hapo awali wapo tayari kutoa ushirikianao na ili benki iweze kutoa pesa wakulima wanapaswa kukubaliana na Mkulazi juu ya mbegu watakazotumia, pili watatakiwa kukamilisha ukomo wa madeni wa vyama vya Ushirika -AMCOS, tatu kuwepo na taarifa za mkulima mmoja mmoja na shamba analomiliki likiwa na hati miliki zinazotambuliwa na Halmashauri, kuwepo na mkataba mkulima baina ya wakulima na Mkulazi na kwamba vitu vyote vikikamilika benki ya Azania itaendelea kutoa mkopo kwa wakulima.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa