Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka amezindua miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa na shirika la World Vision katika kata za Zombo na Ulaya na kuwataka wananchi kuitunza miradi hiyo.
Miradi iliyozinduliwa ni pamoja miradi ya maji katika vijiji vya Zombo, Ulaya Mbuyuni na Madudumizi, ujenzi wa madarasa manne, Maktaba, jengo la utawala na madawati 120 katika shule ya msingi Madudumizi lakini pia ujenzi wa Zahanati na jengo la mama na mtoto katika kijiji cha Madudumizi ambayo ina thamani ya zaidi ya shilingi milioni 800 huku wananchi zaidi ya 1000 wakitarajiwa kunufaika na miradi hiyo.
Akihutumia katika sherehe za uzinduzi huo uliofanyika katika viwanja vya Zahanati ya Madudumizi June 29, 2024, Mkuu wa Wilaya amelipongeza shirika la World vision kwa utekelezaji wa miradi hiyo na kuahidi kuwa serikali ya awamu ya sita itaendelea kushirikiana na wadau katika kuwaletea maendeleo wananchi.
Aidha amewataka wananchi ambao ni wanufaika wa miradi hiyo kuitunza ili iwe na tija kwao na hata vizazi vya baadae.
Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kilosa, Zakia Fandey ambaye ni Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa amesema kuwa Halmashauri itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wadau wa maendeleo na kuahidi kuwa wao kama Halmashauri wataendelea kufuatilia ustawi wa miradi hiyo.
Akitoa salamu za shirika, Pudensiana Rwezaula ambaye ni Meneja wa shirika hilo kanda ya Kati na Nyanda za Juu Kusini ameshukuru serikali ya Wilaya kwa kuwapa ushirikiano wa kutosha wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo huku akiwapongeza wananchi wa maeneo hayo kwa kuonesha ushirikiano wakati wa kutekeleza miradi hiyo.
Aidha ameutaka uongozi kuendelea kuwatambua watu wenye uhitaji na wenye kipato cha chini kuondolewa gharama za kupata huduma katika miradi hiyo hususani ghama za kupata huduma ya maji ili na wao wanufaike na miradi hiyo.
Naye diwani wa Kata ya Zombo Mhe. Lusinde Eliasi amelipongeza shirika la World Vision kwa Kuwaletea wananchi wake miradi hiyo ambayo imepunguza uhitaji kwa kiasi kikubwa na kuwaomba kuendelea kutekeleza miradi mingine katika maeneo ya kata yake.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa