Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Shaka Hamdu Shaka amefanya ziara yake kwa mara ya kwanza katika kata ya Magubike ikiwa ni muendelezo wa kukutana na wananchi wa kata mbalimbali Wilayani hapa kwa kusikiliza kero za Wananchi wa kata hiyo na kusema kuwa watahakikisha wanatekeleza matakwa ya Ilani ya chama kilichopo madarakani, chama cha mapinduzi (CCM).
Mkuu huyo wa Wilaya amefanya Ziara hiyo juni 22 mwaka huu akiambatana na kamati ya Ulinzi na usalama ya Wilaya hiyo, Katibu Tawala Wilaya bi Salome Mkinga, Pamoja na baadhi ya Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri, kwa kusikiza changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa magubike kwa lengo la kufanyia kazi changamoto hizo.
Mh Shaka amesema kuwa Viongozi wa wilaya ya Kilosa wapo kwa ajili ya wananchi wa Magubike na Kilosa kwa ujumla kwa kuwatekelezea mambo mbalimbali ya nayohusu maendeleo na uchumi kwa wananchi hivyo anaomba ushirikiano kwa viongozi wa wilaya hiyo pamoja na wananchi ili kufanikisha utekelezaji wa ilani ya Chama hicho kilichopo madarakani .
Aidha baadhi ya wananchi wametoa kero mbalimbali zinazowakabili ikiwemo uhaba wa maji, ubovu wa barabara ya mwandi-magubike, kukosekana umeme katika baadhi ya vitongoji, migogoro ya mipaka kati ya kijiji cha ibindo na chaumbere, kukosekana kwa kituo kidogo cha polisi, uhaba wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo katika shule ya msingi magubike, uhaba wa chakula na ukosefu wa Zahanati katika kitongoji cha Mwandi.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya kilosa Dr Yuda Mgeni amesema kuwa wamepokea kero hizo na kuahidi kuzifanyia kazi, ambapo kuhusu uhaba wa chakula amesema kuwa tayari kama Wilaya wameshapitisha timu kwa ajili ya kufanya tathmini ili kubainisha hali ya chakula baada ya kuona mwenendo wa hali ya hewa siyo mzuri na tayari ripoti imekamilika na kuwasilishwa katika mamlaka ya hifadhi ya chakula NRFA hivyo mchakato ukikamilika chakula hicho cha bei nafuu kitaletwa kulingana na mahitaji ya wananchi.
Kwa upande wake Mkuu wa kituo cha polisi Dumila ASP Emmanuel Mabembere ambaye alimwakilisha Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD)ametoa Rai kwa wananchi na madereva wanaotumia vyombo vya moto hususani bodaboda kufuata na kuheshimu sheria za barabarani ili kuepuka ajari zisizo za lazima pia amesisitiza kila mmoja kuwa mlinzi wa mwingine ili kuepuka uhalifu katika maeneo yao.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa