Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka amekemea vikali vitendo viovu vinavyofanywa na baadhi ya wafugaji dhidi ya wakulima kwa kujichukulia sheria mkononi bila kufata utaratibu wa kisheria na kusababisha hali ya uvunjifu wa amani katika makazi ya wananchi wilayani hapo.
Mhe. Shaka ameyasema hayo katika ziara yake ya siku mbili zilizofanyika tarehe 20 na 21 septemba, 2023 ambapo amesikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa kata ya mikumi kitongoji cha mbegesera sambamba na kata ya Masanze kitongoji cha Dodoma isanga ambapo wananchi walipata nafasi ya kuzungumza changamoto zinazowakabili kama vile migogoro ya wafugaji na wakulima.
Katika mikutano hiyo ya hadhara Mhe. Shaka amesema kuwa tayari zipo hatua za awali ambazo zimeshachukuliwa kwa ajili ya kutatua changamoto hizo na bado Serikali inaendelea kuchukua hatua stahiki katika kutatua migogoro ya wafugaji ambayo ni tatizo kubwa katika kata hizo na kuhakikisha wananchi wanaishi kwa utulivu, amani na usalama.
Aidha Mhe. Shaka amesema kuwa hafurahishwi na vitendo hivyo viovu kutoka kwa wafugaji hao ambao wamekuwa tishio kubwa kwa wakulima kwa kuwafanyia kuharibifu wa mazao katika mashamba yao na wakati mwingine kuwajeruhi kwa kutumia silaha za jadi na kusababisha uchumi wao kudidimia.
Sambamba na hayo Mhe. Shaka amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano wao kwa jeshi la polisi ili kutokomeza vitendo hivyo viovu na kuendelea kuiamini serikali yao ambayo lengo lake ni kuhakikisha ulinzi na usalama ni haki ya kila mwananchi.
Naye Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo Dkt. Yudah Mgeni amesisitiza wananchi kuishi kwa kuzingatia mpango wa matumizi bora ya ardhi kwani wananchi wote wanategemeana na hakuna aliyebora zaidi ya mwingine.
Akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Contantine Nzila amesema kuwa migogoro hiyo inayosababishwa na wafugaji bado ni changamoto katika vitongoji hivyo, kitu ambacho ni tishio kwa usalama wa wakulima pamoja na mali zao hivyo kwa kushirikiana na viongozi wengine na wadau mbalimbali watahakikisha migogoro hiyo inatatuliwa kwa kufata utaratibu wa kisheria.
Mbali na migogoro ya wafugaji na wakulima pia wananchi hao walibainisha kero mbali mbali kama vile kuchelewa kufika kwa huduma ya umeme, ukosefu wa maji pamoja na ubovu wa barabara kutoka miyombo mpaka Dodoma isanga kata masanze ambayo ina umbali wa km.10.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa