DC Kilosa aagiza zahanati kujengwa kwa mwezi mmoja
Posted on: June 29th, 2022
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Alhaj Majid Mwanga ameupa mwezi mmoja uongozi wa kata ya Kimamba A kuhakikisha ujenzi wa zahanati unafanyika katika kijiji cha Kimamba ili kutatua kero hiyo ambayo ni ya muda mrefu.
Hayo yamejiri Juni 28 mwaka huu wakati Mkuu huyo wa Wilaya akiwa kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji hicho ili kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua ambapo kero mmojawapo ikiwa ni kijiji hicho kukosa zahanati kwa muda mrefu.
Mh. Majid amesema ukosefu wa zahanati kijijini hapo ni suala la aibu na sio vema kuona wananchi wanateseka kwa kukosa huduma za afya kwa kukosekana kwa zahanati huku akiutaka uongozi wa kata hiyo kusimamia zoezi hilo lakini pia amewataka wananchi kushirikiana kwa pamoja ili kukamilisha ujenzi huo.
Aidha amewataka wananchi kufanya harambee ya kuchangia ujenzi huo kwa kila kaya kutoa mfugo mmoja kama kuku ili kuweza kuharakisha kukamilika kwa jengo hilo ambapo ameahidi kushirikiana na Serikali kuhakikisha umaliziaji unafanyika kwa haraka.
Hatahivyo amemtaka afisa mtendaji wa kata kushirikiana na mwenyekiti wa kijiji kuhakikisha wanasimamia vizuri zoezi hilo la harambee na ndani ya mwezi mmoja jengo liwe limekamilika na kwamba wananchi wahakikishe Agosti 23 mwaka huu wanahesabiwa ili kuirahisishia serikali katika upangaji wa bajeti kwa maendeleo ya taifa.