Washiriki wa mafunzo kwa wakulima na wajasiliamali wadogo wadogo katika kata ya Mvumi wameshauriwa kujiunga katika ushirika lakini pia kuchapa kazi kupitia mafunzo waliyojifunza sambamba na kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais wa awamu ta Tano kwa kuanza kuzalisha mazao mengi kwa ajili ya majiji makubwa kupitia fursa ya reli ya mwendo kasi kwani kunatarajiwa kuwa na soko kubwa katika jiji la Dodoma na Dar es salaam.
Ushauri huo umetolewa na Katibu Tawala Wilaya Yohana Kasitila wakati wa kufunga mafunzo kwa wakulima na wajasiliamali wadogo wadogo wa vijiji vyan Mvumi na Gongwe yaliyoendeshwa chini ya uwezeshaji wa MKURABITA ambapo wametakiwa kutumia vyema mafunzo waliyoyapata ikiwemo kutumia fursa ya kuunganishwa na taasisi za kibenki kwa kufungua akaunti na kuweka akiba kupitia miradi mbalimbali watakayoiendesha baada ya mafunzo hayo.
Kasitila amepongeza vijiji hivyo kwa kuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa kurasimisha mashamba yao ambapo amesema kuwa ni vema wananchi hao wakatumia fursa mbalimbali zinazojitokeza kupitia vikundi, ushirika na mkulima mmoja mmoja kwani hati miliki walizonazo baada ya kurasimisha mashamba zina faida kubwa ikiwemo kuwa na usalama wa miliki kwa kuiongezea thamani ya ardhi, kutumika katika mahakama mbalimbali kama dhamana, kupata mikopo katika taasisi za kifedha ambapo hati zinaweza kutumika kama dhamana na kupata fedha kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo kusomesha watoto na mambo mbalimbali.
Aidha amewataka kuwa chachu ya kuleta mabadiliko katika kata ya Mvumi kwa kuanza kubadilika kimtazamo kwa kuyafanyia kazi mafunzo waliyojifunza ili kupata tija katika maisha katika maeneo mbalimbali ikiwemo kujenga nyumba za kisasa, kukidhi matibabu na mahitaji mbalimbali ya kifamilia.
BAADHI YA WANANCHI WA KATA YA MVUMI WALIOPATA MAFUNZO WAKIMSIKILIZA MGENI RASMI
Pamoja na hayo amewataka wananchi kutambua kuwa zoezi la Uboreshaji daftri la Kudumu la Wapiga Kura, hivyo wananchi ambao hawajajiandikisha na wale wenye uhitaji wa kuboresha taarifa zao kuvifika katika vituo kwa ajili ya kujiandikisha na kuboresha taarifa zao ambapo zoezi linategemewa kufanyika wilayani Kilosa kwa siku saba kuanzia tarehe 03/02/2020 na kufika tamati tarehe 09/02/2020 ili kutopoteza haki ya kikatiba ya kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa