Wakulima wa kata ya Mvumi wametakiwa kutambua kuwa fursa ni uwezekano wa kufanya kitu au jambo halali kwa lengo la kuongeza kipato katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo au biashara ambapo katika kilimo wametakiwa kufanya kilimo biashara kwa kuwa na matokeo chanya ya kitu wanachotaka kukifanya katika mtazamo wa kupata faida.
Hayo yamebainishwa na Anthony Temu Meneja Urasimishaji Rasilimali Ardhi Vijijini toka Ofisi ya Rias MKURABITA ambapo ameseama ni vema kuwa na mtazamo wa kupata faida kabla ya kufanya jambo kwa kuwa na uwezo wa kupanga kabla ya kufanya ambapo amesema kuwa tatizo ni fursa hivyo yanapojitokeza mtu anapaswa kuwaza na kupanga namna ya kulitatua kwa kulenga kupata faida.
Temu amewataka washiriki wa mafunzo hayo kutambua kuwa kila aliyefanikiwa lipo jambo alilofanya hivyo amewataka kuwa na mtizamo chanya na kuwa na wivu wa maendeleo hivyo ni vema watu wakawa wadadisi wa kutaka kujua mambo na kujifunza kupitia watu wengine ikiwemo kutafuta taarifa mbalimbali.
Temu amesema fursa zinaweza kutambuliwa kwa kupitia ongezeko la watu kwani watu ni soko lakini pia ni uchumi kupitia mahitaji mbalimbali ya jamii ambayo inaongezeka hivyo mtu anaweza kutumia fursa ya ongezeko la watu kutoa huduma kupitia mahitaji yao lakini pia amewataka kutambua kuwa uwepo wa miradi ni sehemu ya fursa kwa kuangalia nini cha kufanya ili kupato kipato tofauti.
Sambamba na hayo amesisitiza uthubutu wa kutumia fursa husika lakini pia kutumia ukuaji wa uchumi kama fursa kwani kadri uchumi unavyokuwa ndivyo na mzunguko wa fedha ulivyo hivyo amewataka washiriki hao kujua namna ya kuizuia fedha na kuifanya ikae mikononi mwao kwa kuwa na mtizamo wa kujiwezesha kiuchumi na kuwa wajasiliamali kwa kuangalia namna kujipatia kipato .
Akizungumzia suala la ujasiriamali Temu amesema ujasiriamali ni ule mshawasha wa kupata mali hivyo ili kufanikiwa ni lazima kuwe na ujasiri katika kutafuta mali na kubadili mtazamo kwa kuwa na uwezo wa kutambua kwa haraka changamoto na kuzifikiria na kuzigeuza fursa kwa kuwa na ubunifu kwani mjasiriamali ni lazima awe tofauti na mwepesi wa kubuni mambo kwa faida.
Aidha amewashauri kabla ya kufanya jambo kutafuta utaalam dhidi ya jambo wanalopanga kulifanya ili kupata elimu juu ya jambo husika ili pindi wanapoamua kufanya jambo wawe na elimu ya jambo husika jambo litakalowasaidia kulifanya kwa ufasaha zaidi.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa