Mwanamke ni msingi wa mabadiliko katika familia hivyo anapaswa kushirikishwa katika kufanya maamuzi ambapo wanaume na wanawake wanapaswa kushirikiana katika kazi za Maendeleo ya familia lakini pia ipo haja ya kukumbushana umuhimu wa kizazi cha usawa katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu katika ngazi zote za kuamua, kupanga, kutekeleza na kutathmini katika mipango yetu ya kila siku ili kuinua kipato katika familia.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Christina Hauli katika maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa Machi 8 kila mwaka ambapo Kauli mbiu ya mwaka huu 2020 ni “Kizazi cha Usawa kwa Maendeleo ya Tanzania ya Sasa na Baadaye”. Kauli mbiu inayolenga kuelimisha, kuhimiza na kuhamasisha umma kuhusu umuhimu wa usawa wa kijinsia katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu .
Hauli amesema maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ni mojawapo ya mkakati wa Serikali katika kujenga uchumi na Taifa linalojitegemea kuelekea uchumi wa kati, kwa misingi ya utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia (2000), na Dira ya Taifa ya Maendeleo (2025) ni mojawapo ya miongozo ya Serikali unaotoa mwelekeo wa kushughulikia maendeleo ya wanawake kwa kutumia kizazi cha usawa, sera ambayo inatambua umuhimu wa maendeleo ya uchumi kijamii, kisiasa na kiutamaduni kwa wananchi wa jinsi zote.
Aidha amesisitiza viongozi katika ngazi mbalimbali kuwa chachu na wahimizaji wakuu katika utekelezaji wa Seraambao unatilia mkazo uchambuzi wa kijinsia kuwezesha uingizaji wa masuala ya kizazi cha usawa katika mipango, program na miradi ya maendeleo ambapo jamii ikielimika vilivyo, siku ya Wanawake hatutazungumzia matatizo na vikwazo vya kinamama badala yake tutakuwa tukipima maendeleo yaliyofikiwa kwa nguvu zao kupitisha mipango yao.
Hatahivyo Hauli amesema Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa inatambua kikamilifu kwamba wanawake na wanaume wana mchango mkubwa sana katika mipango na miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ambapo kwa kuamini hivyo wanaume na wanawake wana jukumu na wajibu katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo kwa lengo la kuinua kipato cha kaya na taifa kwa ujumla.
Pamoja na hayo Hauli amesema licha ya jitihada nyingi kufanyika bado kuna vitendo vya unyanyasaji na ukiukwaji wa haki za binadamu na hususani haki za Wanawake ambapo ametaka kutumika kwa vyombo mbalimbali vya msaada ili kupunguza changamoto hizo ikiwemo Dawati la Jinsia kupitia Polisi, wasaidizi wa kisheria Paralegal, TAMWA pamoja na Ofisi za Ustawi wa Jamii.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa