Usimamizi mzuri wa matumizi ya fedha za mapato ya ndani pamoja na nidhamu ya matumizi pamoja kupunguza matumizi yasiyo ya lazima vimekuwa msaada mkubwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa katika kuhakikisha inakuwa na miradi ya maendeleo ambayo imekuwa ikifanyika katika kata mbalimbali zilizopo wilayani Kilosa na kuifanya wilaya kuwa na hati safi kwa miaka mitano mfululizo ikiwa ni miongoni mwa halmashauri chache zilizofanya vizuri.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mh Hassan Mkopi wakati wa ziara ya kamati ya fedha, uongozi na mipango iliyokuwa ikitembelea miradi mbalimbali ambapo amesema kuwa kupitia mapato ya ndani sambamba na uwezeshaji wa fedha toka serikalini Halmashauri imefanikiwa kuwa na miradi mbalimbali katika sekta mbalimbali ikiwemo utoaji wa asilimia kumi kwa vijana, wanawake na wenye ulemeavu jambo linalosaidia kwa kiasi kikubwa halmashauri kusonga mbele.
Mkopi amesema anamshukuru sana Mheshimiwa Rais wa awamu ya tano kwa kuitazama Kilosa kwa mapana yake na kuipatia fedha kwa nyakati tofauti tofauti ili kusukuma mbele maendeleo katika wilaya katika sekta ya afya, elimu, kilimo lakini pia amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambmable na timu yake kwa ushirikiano waliouonyesha kwa kuhakikisha fedha zinatengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo ambapo wamekuwa wakishirikiana na waheshimiwa madiwani katika kuhakikisha miradi hiyo inakuwa bora na inayokidhi viwango.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale amemshukuru Mheshimiwa Rrais wa awamu ya tano kwa namna ambavyo amekuwa akishirikiana na Wilaya ya Kilosa kwa kuipatia fedha mbalimbali katika miradi inayoendelea jambo ambalo limesaidia kwa kiasi kikubwa kusukuma mbele guruduma la maendeleo ambapo fedha hizo zimekuwa zikitumika katika miradi ya sekta ya afya, miundombinu ya umwagiliaji na miradi mingineyo.
Pamoja na hayo Mwambambale amesema Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imefanikiwa kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais wakati alipotembelea wilaya ya Kilosa Machi 13 mwaka huu na kuagizwa kujengwa jengo la upasuaji katika kituo cha afya Magubike agizo ambalo limetekelezwa ambapo kwasasa jengo hilo limekamilika na kujengwa kwa fedha za mapato ya ndani na kugharimu kiasi cha shilingi milioni 103 ambazo zimetumika lengo ikiwa ni kudhibiti matumizi na kuokoa fedha za Serikali ambapo wilaya imekuwa ikifanya hivyo katika miradi mingine inayoendelea ikiwemo ujenzi wa wodi mbili za wanawake na waume katika kituo cha afya Mikumi wodi ambazo kwa kiasi kikubwa ziko katika hatua za mwisho.
Akibainisha baadhi ya miradi mbalimbali ambayo imefanyika na inayoendelea kupitia mapato ya ndani Mwambambale amesema miradi hiyo ni ujenzi wa wodi mbili za kituo cha afya Mikumi, jengo la upasuaji kituo cha afya Magubike, ujenzi wa kituo cha afya Mvumi, ujenzi wa madarasa shule ya msingi Msowero huku akisema kuwa Halmashauri imejipanga kuongeza zaidi matumizi katika miradi ya maendeleo kwa kufikia 60% huku matumizi ya kawaida ikiwa 40% huku akisisitiza kuwa shauku ya Halmashauri kuwa na miradi ambayo thamani yake inaonekana kwa macho zaidi.
Aidha katika ziara hiyo Mwenyekiti wa kamati ya huduma za jamii Mh Abdullatif Kaid amepongeza Halmashauri na Serikali kiujumla kwa juhudi mbalimbali ambazo zimekuwa zikionekana katika kuleta maendeleo kwa wananchi ambapo wananchi kiujumla katika kata zenye miradi ya afya wameshukuru kwa ujenzi wa majengo ambalimbali ya kutolea huduma unaoendelea kwani kwa kiasi kikubwa utawaondolea adha kwenda kutafuta huduma za afya maeneo ya mbali jambo linalowagharimu muda, matumizi ya fedha nyingi na kutembea umbali mrefu.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa