Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Mipango, Takwimu na Ufatiliaji Francis Kaunda ameushukuru uongozi wa benki ya NMB kwa juhudi zake za dhati katika kuunga mkono shughuli za maendeleo katika sekta ya elimu kwa kukabidhi madawati 70 yenye thamani ya shilingi milioni tano katika shule ya Msingi Msowero.
Kaunda ametoa shukrani hizo Juni 07 mwaka huu wakati wa makabidhiano ya madawati hayo ambapo amesema kuwa halmashauri inaahidi kuyatunza madawati hayo lakini pia amezitaka shule mbalimbali kuendelea kujenga vyumba vya madarasa ili kuweza kukidhi mahitaji na kwamba Serikali ya awamu ya Tano na Halmashauri iko bega kwa bega katika ujenzi huo kwa kuhakikisha vyumba hivyo vinakamilika na wanafunzi kupata mazingira mazuri ya kujifunzia.
Kaunda amesisitiza ujenzi wa maboma kwani licha ya Serikali kuweka nguvu yake katika ujenzi huo lakini pia amesema wapo wadau mbalimbali wa elimu wakiwemo NMB ambao wako tayari kuunga mkono juhudi zinazofanyika kwa kuhakikisha licha upatikanaji wa vyumba vya madarasa vilivyokamilika lakini pia upatikanaji wa madawati, meza, viti na mabati vinapatikana.
Naye Meneja Mahusiano Biashara ya Serikali kanda ya Mashariki Anneth Kwayu kwa kushirikiana na Meneja wa NMB tawi la Kilosa Assey Mfinanga wamesema NMB ni mdau wa maendeleo hivyo wanao wajibu wa kuchangia shughuli za maendeleo na kwamba kwao kuchangia sekta ya elimu ni jambo la kipaumbele ikiwa ni sehemu ya kurejesha sehemu ya faida kwa jamii kwa kuhakikisha changamoto za jamii zinapatiwa ufumbuzi kwa kujenga afya bora na elimu bora kwa jamii ya kitanzania huku wakisistiza Ofisi ya Mkurugenzi kutosita kuwashirikisha katika shughuli za maendeleo hasa katika sekta ya afya na elimu.
Aidha Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi Christina Hauli ametoa wito kwa wazazi katika shule mbalimbali za msingi hasa zinazotarajia kuwa na makambi kwa ajili ya wanafunzi wa darasa la saba ili kuwa na muda mzuri wa kujisomea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa uongozi wa shule kwa kuhakikisha watoto wao wanakuwa katika mazingira mazuri ya kujisomea na kupata chakula cha kutosha kwa wanafunzi ili kuwa na chachu ya ufaulu na kuiletea sifa wilaya ya Kilosa kwa kuwa na kiwango kizuri cha ufaulu.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa