Naibu Katibu Mkuu CCM Bara ambaye pia ni mlezi wa mkoa wa Morogoro Mh Rodrick Mpogolo ametoa wito kwa uongozi wa Halmashauri kuongeza bidii katika ujenzi wa kituo cha afya Mikumi ili huduma za afya zianze kwani eneo hilo ni eneo lenye wakazi wengi, hivyo linastahiki kuwa na kituo cha afya ambapo huduma za afya zitakapoanza zitakua na manufaa kwa wananchi.
Aidha Mpogolo ametoa rai kwa watumishi wa afya pamoja na watumishi wa umma kwa ujumla kutoa huduma stahiki zenye ufanisi kwa wananchi pasipo kuomba rushwa kwani ni jambo la faraja kwa wananchi kupata huduma za afya katika hali nzuri ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Mh Rais kwa kuwajali wananchi.
Sambamba na hayo ametoa pongezi kwa wananchi kwa namna walivyoshiriki katika ujenzi wa kituo hicho kwa kushiriki katika shughuli mbalimbali ikiwemo kuchimba msingi, kumwaga zege la msingi na jamvi, ujazaji vifusi kwa majengo yote manne ambapo kiujumla nguvu za wananchi zilizotumika zimegharimu shilingi 15,103,240.000.
Naye sambamba na hayo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe S. Kebwe ameishukuru Serikali ya awamu ya Tano kwa ajili ya kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya maendeleo ya wananchi huku akisisitiza ujenzi katika vituo vya afya mkoa wa Morogoro kuendelea kufanyika usiku na mchana na kwamba upatikanaji wa dawa uko vizuri, huku Mbunge wa jimbo la Kilosa Mh. Mbarak Bawazir amesema kuwa kutokana na changamoto ya maji ataongeza nguvu kwa kuchimba kisima ili maji yaweze kupatikana muda wote kwani eneo hilo ni eneo linalohitaji huduma za maji muda wote na ya kutosha.
Akisoma taarifa yake kwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara Mganga Mkuu wa Halmashauri Dkt. Halima Mangiri amesema kuwa katika kutekeleza azma ya kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya Serikali imetoa shilingi milioni 400 kwa ajili ya kujenga/kukarabati majengo katika kituo cha afya Mikumi ambapo mradi huo umejumuisha jengo la upasuaji, wodi ya wazazi, maabara na jengo la wagonjwa wa nje na kwamba Halmashauri ianatarajia kusimamia mradi ukamilike kwa wakati sambamba na kuendelea kuhamamsisha na kuelimisha wananchi ushiriki wao katika miradi ya maendeleo.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa