Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Prof Palamagamba Kabudi ametoa agizo kwa Afisa Ardhi wa Wilaya ya Kilosa na wa Mkoa wa Morogoro kupima eneo lote la Kituo cha Maendeleo Dakawa na mchakato wa kutoa hati miliki kisheria ukamilike na eneo lote la kituo ambalo halina mgogoro liwekewe uzio ili watu wasivuke na kufanya uvamizi.
Mhe. Prof Kabudi ameyasema hayo 08 Februari 2025 akiwa katika ziara yake ya kikazi ya siku moja Wilayani Kilosa ya kutembelea maeneo ya kihistoria katika Kituo cha Maendeleo Dakawa ambapo Mhe. Prof Kabudi amesema kuwa eneo ambalo lina mgogoro na lipo mahakamani waendelee kulishughulikia ili haki itakapopatikana utaratibu mwingine uendelee wa namna sahihi ya umiliki wa eneo hilo.
“Maeneo haya yapewe hati serikali ni moja sera ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuyalinda maeneo haya kwa matumizi ya leo lakini akiba kwa matumizi ya kesho”. Alisema Prof. Kabudi
Pia Prof. Kabudi amesisitiza kwa baadhi ya wananchi wanaoishi maeneo ya jirani na Kituo cha Dakawa kuacha kufanya uvamizi kwenye maeneo mbalimbali ya badala yake watafute utaratibu unaofaa kupata maeneo ya ardhi watakayoyatumia kwa matumizi mbalimbali.
Sambamba na hayo ameongeza kuwa zinatanza jitihada za baadhi ya maeneo ya kumbukumbu za wapigania Uhuru kama vile Dakawa, Mazimbu, Kongwa, Mgagao, Nachingwea na Bagamoyo yaingizwe katika sehemu ya urithi wa dunia chini ya shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) ili kuendelea kuwa na kumbukumbu zenye thamani na kuongeza utalii katika eneo hilo.
Mhe. Prof Kabudi amesema kuwa litajengwa jengo ili kuweza kuanzishwa kituo cha taarifa ili kufanya Wilaya ya Kilosa kama sehemu muhimu ya utalii wa kihistoria hivyo ameendelea kuwaasa wananchi kuacha kufanya uharibifu wa maeneo hayo kwani wakiyalinda yatawasaidia kwa matumizi ya baadae.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa