Mgombea wa nafasi ya ubunge kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi Profesa Palamagamba Kabudi Agosti 27 mwaka huu amewashukuru wanakilosa kwa dhamira ya dhati na imani waliyoonyesha ya kumwamini na kuridhia aliongoze jimbo la Kilosa Mjini mara baada kupita bila kupingwa huku akiwataka kutambua kuwa dhamira yake kuiongoza Kilosa ni kwa ajili ya kushirikiana na wanakilosa katika kutatua changamoto kwa pamoja.
‘’Sijaja Kilosa kutatua changamoto zenu bali nmekuja kutatua changamoto zetu yaani changamoto zangu na zenu hivyo napenda mfahamu nmekuja kushirikiana nanyi ili tutatue changamoto zetu kwa pamoja kwani nimedhamiria kuwa mtumishi wenu’’ Kabudi amesema.
Kabudi amesema kwa dhati ataitumikia Kilosa na kushirikiana na wanakilosa kutatua changamoto zilizopo huku akisema kuwa baada ya kufikia maamuzi ya kuwania nafasi ya ubunge alitembelea kata 25 ili kuijionea uhalisia hususani katika miundombinu ya barabara ambapo baada ya kujionea tayari baadhi ya barabara katika kata za Lumbiji, Berega, Mabula, Magubike, Lumuma na Mamboya ziko vizuri.
Aidha amemshukuru Mungu kwa kumheshimisha lakini pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa namna alivyomwamini na kumteua kuwa mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki huku akitaja baadhi ya mikataba mbalimbali aliyowahi kuishughulikia kam waziri na kuleta tija kwa taifa hivyo anaamini wakati umefika wa kushirikiana na wanakilosa pasipokujali kabila, dini wala itikadi za vyama kwani maendeleo ni kwa ajili ya kila mwanakilosa.
Sambamba na hayo amesema ili kuwa na Kilosa mpya ya matumaini mapya ameomba ushirikiano wa dhati ili kufanya kazi pamoja ikiwemo kubaini tunu mbalimbali zilizopo Kilosa kama vile uwepo wa reli ambayo ni injini ya maendeleo huku akibainisha mambo mbalimbali yaliyopo katika ilani kwa tija ya Kilosa kama vile umaliziaji wa baadhi ya barabara kama ya Kilosa- Mikumi na nyinginezo, kuwepo kwa miradi ya maji, mradi wa ufugaji wa kisasa, utotoaji vifaranga vya kuku kwani reli zitakapokamilika mahitaji mbalimbali yataongezeka na kuwa Wilaya ya Kilosa ni ya kimkakati.
Naye mgombea wa jimbo la Mikumi kupitia CCM Denis Londo amesema amefarijika kwa heshima kubwa waliyoionyesha wanakilosa husasni kwa mgombea wa jimbo la Kilosa kupita bila kupingwa kwani Profesa Kabudi ni tunu na kwamba anaamini ifikapo Oktoba 28 heshima ya jimbo la Mikumi, Kilosa na mkoa wa Morogoro vitarejea na wamejiandaa kujibu changamoto za wananchi kupitia ilani ya uchaguzi ya CCM ambapo pia Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi akitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi pindi Mheshimiwa Rais atakapofanya kampeni zake wilayani Kilosa zinazotarajiwa kufanyika katika kata ya Dumila na Kilosa mjini pindi itakapotangazwa ili waweze kusikiliza sera za CCM.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa