Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) kuwapa kipaumbele wakandarasi wazawa ili kuwajengea uwezo na kukuza uchumi wao na nchi kwa ujumla.
Mhe Rais ametoa kauli hiyo 3 Agosti,2024 katika uwanja wa Shule ya Msingi Kilosa Town wakati akizungumza na Wananchi baada ya kuzindua barabara ya Rudewa -Kilosa yenye urefu wa km 24 ambayo ujenzi wake umeghalimu kiasi cha shilingi Bilioni 45.6.
Mhe. Samia amesema kuwa endapo mkandarasi mzawa atapewa kazi na kupata malipo ya kazi hiyo atatumia fedha hizo kununulia bidhaa na kulipa posho za vibarua lakini pia atazitumia fedha hizo katika matumizi mbalimbali ya kawaida na kupelekea fedha hizo kuzunguka ndani ya nchi.
Aidha Rais Samia ameongeza kuwa Mradi huo wa barabara utarahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji kwa wananchi na bidhaa zao hivyo, kushamiri kwa biashara na kupandisha uchumi wa Kilosa.
Katika hatua nyingine, Mhe. Rais ameipongeza TANROADS na wakandarasi wazawa kwa kukamilisha mradi huo wa barabara ambao utaleta tija kwa wananchi na kuwataka wananchi kuitunza miundombinu yote iliyotekelezwa wilayani hapo.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa