Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima ameitaka Halmashauri ya wilaya ya Kilosa kuyapa kipaumbele mazao ya kimkakati kama vile kokoa ili kuinua uchumi wa wananchi na pato la Halmashauri kwa ujumla.
Mhe. Malima ametoa rai hiyo wakati wa mkutano maalumu wa baraza la madiwani wa kujadili taarifa ya utekelezaji wa mapendekezo ya mdhibiti na mkaguzi wa fedha za serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2022/2023 uliofanyika June, 25, 2024 katika ukumbi wa Chuo cha Maendeleo (FDC) Ilonga.
Amesema kuwa kuna haja ya kuwafundisha wananchi namna bora ya kulima mazao hayo ili yawe na tija kwao huku akitaka mifumo maalumu ya kuuza na kununua kama vile Stakabadhi Ghalani ifuatwe ili wakulima wanufaike.
Katika hatua nyingine, RC Malima amezipongeza Halmashauri za mkoa wa Morogoro kwa kuwa na hoja chache zinazoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi wa Serikali (CAG) na kuwataka watendaji pamoja na Waheshimiwa Madiwani kukaa mara kwa mara kuzipitia hoja zilizoibuliwa na kuzimaliza.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mussa Ali Musa amewataka wananchi wa Kilosa kuchangamkia fursa za Uwekezaji katika mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) ambayo itaanza kutumika hivi karibuni huku akiwataka viongozi wa wilaya kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji.
Amezitaja fursa kama vile vituo vya magari, migahawa, hoteli na kadharika kuwa zinaweza kuwa chachu ya maendeleo kutokana na kuwepo kwa reli hiyo.
Naye mkuu wa wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia wilaya ya Kilosa miradi mingi ya maendeleo na kuahidi kuendelea kuisimamia vizuri ili iwanufaishe wananchi wa Kilosa.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mapendekezo ya CAG kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kilosa Michael J. Gwimile amesema kuwa Halmashauri ilifanikiwa kupata hati safi ikiwa ni mwaka wa tisa mfululizo.
Aidha amesema kuwa mpaka mpaka sasa hoja takribani 5 ndizo zilizosalia kati ya hoja 12 zilizoibuliwa na CAG kwa mwaka wa fedha 2022/2023 na kuahidi kuwa hizo zilizobaki zitatatuliwa.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa