Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adamu Kighoma Malima amewataka wafanyakazi kufanya kazi kwa juhudi na maarifa huku wazithamini na kuzi heshimu kazi zao ikiwa ni pamoja na kuacha vitendo visivyo vya kinidhamu kazini kama vile wizi na uvivu.
Ametoa kauli hiyo wakati akihutubia Wafanyakazi na Wananchi kwa ujumla katika Maadhimisho ya siku wa Wafanyakazi Duniani Mei Mosi, 2024 ambayo Kimkoa yamefanyika mjini Ifakara ambapo pamoja na mambo mengine amesema kila Mfanyakazi anapaswa kuwa mwangalizi na mshauri wa mwenzake ili kuleta tija katika kituo cha kazi na Taifa kwa ujumla.
Akijibu Hoja zilizosomwa kwenye Risala ya Wafanyakazi amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita imekuwa ikifanya Jitihada mbalimbali za kuboresha Sekta ya ajira ikiwa ni pamoja na kuajiri watumishi wapya,kupandisha vyeo,lakini pia kuanzisha Mahakama Kuu kanda ya Morogoro ili kusikiliza na kutatua mashauri na kesi mbalimbali kuhusiana na ajira na Watumishi ndani ya Mkoa wa Morogoro.
Mhe. Malima pia amemwagiza Kamishna wa Kazi Mkoa wa Morogoro kupita mara kwa mara kwenye maeneo ya kazi ili aweze kujua changamoto zinazowakabili wafanyakazi lakini pia kumaliza migogoro ihusuyo Mikataba ya ajira.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewapongeza Wafanyakazi waliotunukiwa vyeti vya utumishi Hodari na kuwataka kujituma zaidi ili kutoa hamasa kwa wenzao.
Akitoa salamu za Mei Mosi, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA)Mkoa wa Morogoro Jumanne Nyakirang’ani amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo,Aidha amewashukuru waajiri wote ndani ya Mkoa kwa kuendelea kushirikiana vyema katika kutatua changamoto za wafanyakazi.
Akisoma Risala kwa Mgeni rasmi Nicolaus Ngowi ambaye ni Mratibu wa TUCTA Mkoa wa Morogoro amezitaja hoja ikiwa ni pamoja na kuitaka Serikali kupunguza kodi kwa Waajiri hususani sekta binafsi, kufanyika upya kwa majadiliano juu ya kikokotoo, kadhalika Bima za Afya kwa Wastaafu na uwepo wa Mikataba rasmi kwa Wafanyakazi wa Sekta binafsi pamoja na kuchelewa kwa suluhu juu ya Migogoro ya Wafanyakazi.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa