Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adamu Malima amefanya ziara katika kata za Rudewa na Mvumi Wilayani Kilosa ili kujionea madhara yaliyosabaishwa na mafuriko yaliyozikumba kata hizo usiku wa kuamkia Disemba 05,2023 na kuahidi misaada ya kibinadamu ikiwemo chakula na huduma za afya kwa wahanga wa mafuriko hayo.
Mhe. Malima amefanya ziara hiyo Disemba 06,2023 na kueleza kuwa serikali ya mkoa itachangia mahitaji kama vile chakula, malazi, mavazi kama sehemu ya kuwasaidia waathirika wa mafuriko hayo.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa ameziagiza mamlaka za TANESCO, TARURA, RUWASA na Mamlaka za barabara kurejesha huduma za maji, umeme na miundombinu ya barabara ili kuwaezesha wakazi wa maeneo hayo kurejea katika maisha yao ya kawaida.
Hata hivyo, amesema kuwa katika tathimini ya awali iliyofanywa na kamati ya maafa ya wilaya imebainisha kuwa zaidi ya nyumba 100 zimeathirika na mafuriko hayo huku watu watatu wakifariki kutokana na mafuriko hayo.
Mkuu huyo wa Mkoa pia ametahadharisha baadhi ya watu wanaowaibia wahanga vitu na mali zao kuacha mara moja tabia hizo na kuziagiza mamlaka za ulinzi na usalama kulifanyia kazi suala hilo.
Katika kulikabili hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka ambaye aliambatana na Mkuu wa Mkoa katika ziara hiyo amebainisha kuwa kwa kushirikiana na mamlaka za polisi watahakikisha wanawadhibiti watu wenye nia ya kuwaibia waathirika wa mafuriko hayo
Kwa upande wake Meneja wa mamlaka ya maji safi na salama Mkoa wa Morogoro (RUWASA) Mhandisi Sospita Mtondwa amesema kuwa wameshachukua hatu za awali za kuhakikisha maji yanayopatika katika maeneo yalioathirika na mafuriko ni safi na salama kwa kuweka dawa kwenye maji yaliyotuama ili yasilete madhara kwa watu. Amefafanua kuwa hakuna miundombinu ya maji iliyoathiriwa na mafuriko hayo.
Naye Meneja wa Mamlaka ya Umeme (TANESCO) Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Fadhili Chilombe amesema kuwa wanafuatilia kwa ukaribu madhara yanayoweza kujitokeza kwa kuweka kituo cha dharura (Emergency) maeneo hayo na kuwataka wananchi wa eneo hilo kuwasiliana naye muda wote iwapo kutakuwa na changamoto ya umeme.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa