Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare amewaagiza viongozi wa Wilaya ya Kilosa kukamilisha haraka ujenzi wa jengo la upasuaji la Kituo cha Afya cha Magubike ambalo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliagiza lijengwe na kukamilika ndani ya miezi miwili kuanzia mwezi Machi mwaka huu maagizo yaliyotolewa wakati alipotembelea ujenzi waDaraja la Kiegeya Wilayani Kilosa baada ya kukatika.
Sanare ametoa agizo hilo Mei 5, mwaka huu alipofanya ziara ya siku moja Wilayani humo iliyolenga kusukuma kutekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli aliyoyatoa Machi 17 mwaka huu alipotembelea ujenzi waDaraja la Kiegeya Wilayani Kilosa baada ya kukatika.
Pamoja na kutoa pongezi kwa viongozi hao katika kutekeleza kwa kiasi kikubwa maagizo ya Mhe Rais, amewaagiza viongozi hao kukamilisha haraka ujenzi wa jengo la upasuaji la kituo cha Afya cha Magubike ambalo kwa sasa lipo hatua ya upauaji ambapo ametaka Halmashauri kuendelea kutafuta vyanzo mbalimbali ili kukamilisha haraka iwezekanavyo jengo hilo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale amesema kwa maandalizi ambayo yamekwisha fanyika kusipotokea mabadiliko ujenzi wa jengo hilo utakamilika mwishoni mwa mwezi huu.
Aidha Sanare alitembelea mradi wa maji wa Berega Mgugu ambao unatekelezwa kwa ufadhili wa nchi ya Marekani na kuwapongeza wananchi kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mradi huo na ametumia fursa hiyo pia kumpongeza mwananchi mmoja Bibi Olivia Chitemo (75) wa Kitongiji cha Gongoni Kijiji cha Belega kwa kujitolea kutoa eneo lake ili lijengwe tenki la maji litakalonufaisha watu zaidi ya elfu tano.
Wakati akikagua utekelezaji wa agizo la Rais la kukarabati daraja la mto Belega Sanare amewapongeza wahandisi waliokuwa wanajenga daraja hilo na kutekeleza kazi hiyo ndani ya siku saba na kusema daraja hilo lina umuhimu wa kipekee kwa kuwa linaunganisha Mikoa mitatu ya Morogoro, Dodoma na Tanga lakini pia limeondoa kero kwa wananchi wanaolitumia kuvuka kwenda Hospitala ya Belega.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wananchi wa Magubike na wanamorogoro kwa jumla kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kwamba ugonjwa wa CORONA kamwe usiwe kisingizio cha wananchi kutoshiriki shughuli za maendeleo, kwani amesema ugonjwa huo haujulikani utakwisha lini na kwamba kinachotakiwa ni kujilinda na kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa Afya na Viongozi wa Serikali.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa