Reli ya mwendokasi (SGR), wilayani Kilosa itaanza shughuli zake za usafirishaji hivi karibuni na kupelekea mabadiliko makubwa ya maendeleo ambapo reli hiyo itarahisisha shughuli za usafirishaji kwa wafanyabiashara na kuinua uchumi wa Kilosa.
Hayo yameelezwa 31 Mei, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka H. Shaka katika Mkutano wa Baraza la Biashara Wilaya ya Kilosa uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa.
Akiongoza Mkutano huo kama Mwenyekiti, Mhe. Shaka amesema reli hiyo ya kisasa yenye vituo vitatu wilayani humo, mara baada ya kuanza shughuli za usafiri na usafirishaji itasaidia kwa kiwango kikubwa kurahisisha masuala ya usafirishaji kwa wafanyabiashara kutokana na changamoto za barabara wilayani humo kwamba si rafiki na zinapelekea kukwamisha baadhi ya shughuli za usafiri.
Pia Mhe. Shaka ameongeza kuwa Wilaya ya Kilosa ni miongoni mwa wilaya inayozalisha mazao ya kimkakati kama vile mkonge, mchikichi, karafuu, miwa nk ambapo amewataka wataalamu kuendelea kuhamasisha wakulima kuzalisha mazao hayo pia kufanya tafiti zenye tija zitakazopelekea uzalishaji kuongezeka ili kuinua kipato cha wakulima na wafanyabiashara.
Kwa upande wake Afisa Biashara Mkuu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro Bi. Flora Yongolo ameshauri kuudwa kwa kamati mbili tendaji ambayo ni kamati kazi itakayosaidia kuongoza katika majadiliano shirikishi ya kimkakati na kikosi kazi cha kuibua fursa za uwekezaji.
Aidha, Mhe. Shaka amewashukuru wadau mbalimbali walioshiriki kwenye mkutano huo na kusema kuwa amepokea ushauri, mapendekezo na maoni mbalimbli yaliyotolewa kwa lengo la kuyafanyia kazi.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa