Imebainika kuwa historia ya maisha ya upotevu wa mazao kwa wakulima wa zao la mpunga inaeekea kufikia ukingoni baaada ya mradi wa RIPOMA yaani Mradi wa Kudhibiti Upotevu wa Mpunga kutoka Uvunaji hadi kwa Mlaji kwa Kuboresha Uvunaji , Uhifadhi , Usindikaji na Kuboresha Masoko kutua mkoani Morogoro katika wilaya za Mvomero na Kilosa.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Msaidizi wa shirika la Helvetas Bw. Daniel Kalimbiya wakati wa uzinduzi rasmi wa mradi huo wilayani Kilosa na kusema kuwa lengo kuu la mradi ni kuchangia maendeleo na kupunguza umaskini wa kipato kwenye ukanda wa SAGCOT kwa kuboresha mnyororo wa thamani na masoko ya zao la mpunga ili kuwanufaisha wakulima wadogo.
’’Wakati wa uendeshaji mradi huu tumejikita zaidi katika kuwajengea uwezo na kutoa mafunzo kwa wadau juu ya maswala ya udhibiti wa upotevu wa mpunga, kuongeza ushiriki wa sekta binafsi na serikali katika maswala yanayohusu udhibiti wa upotevu wa mpunga kwenye mnyororo wa thamani, kujenga uelewa juu ya sera ya taifa ya maendeleo ya sekta ya mpunga na kushawishi uwepo wa sera ya kudhibiti upotevu wa mpunga nchini, kuanzisha na kuwezesha shughuli za kuweka akiba na kukopa kwa makundi ya wazalishaji pamoja na kuboresha mifumo ya uzalishaji wa mpunga maghalani na uboreshaji ama ujenzi wa maghala mapya hasa kwenye maeneo yenye tija ya uzalishaji”. Amesisitiza Kalimbiya
Aidha Kalimbiya amesema kuwa mradi ni wa miaka tatu ulianza Julai 2017 hadi Juni 2020 ambapo unalenga kunufaisha kaya 3000, makundi ya wakulima 100 na jumla ya walengwa wa moja kwa moja 15,000 ifikapo 2020, na kuwa msisitizo wa mradi huu ni kwa wanawake na vijana, ambapo wilayani Kilosa unafanya kazi katika kata za Ludewa, Kilangali, Msowero na Chanzuru huku wilayani Mvomero ukifanya kazi katika kata za Dakawa-Mlali, Mvomero, Mkindo-Hembeti, Sungaji na Mtibwa –Kanga.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe S. Kebwe amelishukuru shirika la Helvetas na kusema kuwa Mkoa wa Morogoro una takribani hekta milioni mbili zinazofaa kwa kilimo na amewataka wakulima kuchangamkia fursa ya kilimo hasa cha mpunga kwani soko la mpunga na mchele lipo la kutosha na kupitia elimu inayoendelea kutolewa na Helvetas kupitia mradi wa RIPOMA anaamini wakulima wengi watainuka kiuchumi na amezidi kusisitiza kuacha uvivu wa kimwili na kiakili kwani wataalam wapo, elimu ni bure, hivyo ni vema tukakubali mabadiliko na kuachana na kilimo cha mazoea ambacho hakina tija...
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa