Sekta ya umma na sekta binafsi ni sekta ambazo zinategemeana hususani katika masuala mbalimbali ikiwemo ukuaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi ambapo Serikali inashughulikia masuala ya kijamii na masuala mengine huku sekta binafsi ikijihusisha zaidi na masuala ya kibiashara.
Hayo yamebainishwa Agosti 26 mwaka huu na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi wakati akifungua kikao cha baraza la biashara ambapo amesema sekta hizo ni sekta zinazotegemeana na kwamba kutokana na mfumo wa kiuchumi wa nchi ya Tanzania biashara kwa asilimia kubwa zinafanywa sekta binafsi huku Serikali ikifanya masuala makuu ya kijamii na kurahisisha shughuli za kibiashara kufanyika.
Mgoyi amesema kupitia baraza la biashara yapo masuala mbalimbali upande wa Serikali na sekta binafsi yamekuwa na changamoto lakini kupitia baraza hilo wadau hukutana na kupata mchango mkubwa wa mawazo ambao hupelekea kupata tija kwa maslahi ya pande zote mbili kwani setkta hizo zinategemeana kwa kiasi kikubwa.
Naye Mtendaji wa chemba ya biashara, viwanda na kilimo Mkoa wa Morogoro Moumin Mwatawala akieleza mwongozo wa baraza la biashara amesema baraza hilo ni jukwaa la rasmi la majadiliano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi linalofanyika katika ngazi ya wilaya. Mkoa na taifa ambapo washiriki wake hutoka pande zote mbili huku akisema kuwa mfumo wa baraza hilo huongozwa na Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa au Rais kulingana na ngazi ya baraza na kwamba majadiliano huongozwa na mwenyekiti ambaye kwa mujibu wa mwongozo hapaswi kufungamana na upande wowote.
Akitoa taarifa ya mfumo wa upimaji wa wazi wa halmashauri wenye lengo la kuweka mazingira wezeshi upande wa biashara Afisa Biashara Wilaya Idrisa Jukulu amesema mfumo huo unalenga kupima uwezo wa Hamashauri na kuzishindanisha kwa kuzingatia vipimo vya vipengele muhimu 12 ikiwemo kiunzi cha kisheria, ushiriki na mwitikio, mazingira ya kibali, kodi na ada, huduma za mamalaka ya Serikali za Mitaa, huduma za maendeleo ya biashara, miundombinu ya mamlaka ya Serikali za Mitaa, mpango wa matumizi ya ardhi, upataji fedha, uongozi na utawala na jinsia na vijana.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa