Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema Serikali ya Awamu ya Sita inatambua mchango mkubwa unaotolewa na watumishi wa umma katika kuwahudumia wananchi na kwani watumishi wa umma ni rasilimali muhimu kwa ustawi wa Taifa.
Hayo yamebainishwa na Mhe. Jenista Mhagama wakati wa ziara yake ya siku moja katika Wilaya ya Kilosa ambapo alizungumza na watumishi lakini pia kutembelea walengwa wa mpango wa kunusuru kaya maskini katika kata ya Mvumi ambapo wakati wa kikao na watumishi wa umma kilicholenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi.
Mhe. Jenista amesema kuwa hatomuonea aibu wala huruma kiongozi yeyote aliyepewa dhamana ya kusimamia rasilimaliwatu ambaye atabainika kukiuka sheria na taratibu za usimamizi wa rasilimaliwatu na kuongeza kuwa, viongozi wenye dhamana ya kusimamia rasilimaliwatu wanapaswa kuiheshimu, kuithamini na kuhakikisha inakuwa kwenye mikono salama kwasababu inategemewa na Serikali kwa kiasi kikubwa katika ustawi na maendeleo ya Taifa.
“Rasilimaliwatu ambayo ndio watumishi wa umma ikisimamiwa vizuri itaisaidia Serikali kutimiza lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kutekeleza mipango na mikakati ya maendeleo katika Taifa, na kwamba watumishi wa umma ndio wanategemewa kutoa huduma bora za afya, kuboresha huduma za maji, kuboresha huduma za elimu, kuboresha huduma za miundombinu pamoja na kilimo.” Mhe. Jenista amefafanua.
Kwa upande wa wabunge wa majimbo yote mawili ya Wilaya ya Kilosa Mh. Prof. Palamagamba Kabudi( Kilosa) na Dennis Londo(Mikumi) wameiomba serikali katika utekelezaji wa mpango wa kunusuru Kaya zenye hali duni kutupia jicho maeneo mbalimbali ikiwemoutatuzi wa changamaoto ya kufikika baadhi ya Vijiji vya mpango na hii ni kutokana na kutokuwepo na miundombinu ya barabara na vivuko ambavyo si rafiki hivyo kusababisha shughuli za mpango na uzalishaji kufanyika kwa kiwango kidogo lakini pia utatuzi wa changamoto ya miundombinu ujenzi wa kivuko cha Nyali pamoja na ukarabati wa barabara inayounganisha Vijiji vya Kigunga, Zombo, Nyali, Madudumizi, Nyameni Zombo na Nyameni yenye urefu wa Kilometa 22.4 ambacho itasaidia kasi ya shughuli za Kilimo cha mazao mbalimbali ili kunufaisha wakazi wapatao 13,485 kufikia huduma ya Afya na Elimu kwa uhakika.
Pamoja na hayo wameomba uwepo wa ujenzi wa Barabara ya Mkulazi –Tankini yenye urefu wa Kilometa 6.4 ambayo itasaidia kuwaunganisha wananchi na shughuli za Kilimo lakini pia ujenzi wa daraja la Nyangara na ukarabati wa barabara yenye urefu wa Kilometa 16 ambayo itaunganisha Vijiji vya Nyangara A na B, Kife na Maguha hii itasaidia kuwaunganisha wananchi na shughuli za uzalishaji wa mazao ya Kilimo na kuweza kufikia huduma za Afya na Elimu wa uhakika.
Akisoma taarifa ya Utekelezaji wa shughuli za mfuko wa maendeleo ya jamii-TASAF katika kijiji cha Mvumi Mtendaji wa Kijiji cha Mvumi Godson Mkasya amesema walengwa wameweza kununua vitu mbalimbali na hivyo kuongeza mzunguko wa fedha ikiwemo kuweza kulima kwa trekta badala ya majembe ya Mkono, kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi katika Kijiji kama vile kilimo, ufugaji na biashara ndogondogo kwa kupitia ruzuku wanazopokea, wanafunzi 55 toka Kaya za walengwa wananufaika kwa ruzuku ya elimu kwa kupata mahitaji ya msingi, hali ya kiuchumi ya walengwa kuboreka na hivyo kuweza kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo pamoja na kuboreka kwa hali ya maisha ya walengwa huku wananchi wakitoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kwa kuendelea kutoa ruzuku za walengwa kupitia Mpango wa kunusuru kaya Lengwa kwani Mpango huu umekuwa mkombozi kwa kaya zenye hali duni kwa Wilaya ya Kilosa.
Akizungumza kwa niaba ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Kilosa, Mwalimu Richard Shagungu ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kulipa kila mwezi madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi katika Halmashauri hiyo na kuomba waajiri wasizalishe madai mapya ili Serikali iyamalize madai yaliyopo sasa.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa