Katika kuhakikisha mazingira ya watumishi yanaboreshwa kama kupandisha mishahara Serikali ya awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan Serikali imekuwa ikijiimarisha uchumi kwa kuanzisha miradi ya kimkakati katika miradi itakayofungua fursa za kiuchumi na kuongeza uzalishaji ili Taifa liweze kupata mapato zaidi.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mheshimiwa Martin Shigela wakati wa siku ya Mei Mosi yenye kaulimbiu ‘’Mishahara na Maslahi Bora Kwa Wafanyakazi Ndiyo Kilio Chetu’’#KAZI IENDELEE ambapo amesema Serikali imeendelea kujenga vituo vya afya, shule za sekondari na msingi, hivyo ni dhahiri Serikali inatambua haja na tija kwa wafanyakazi kupata mishahara mizuri na kuboresha mazingira ya kazi ikiwemo upandishaji wa madaraja, na kwamba imetenga bajeti kwa ajili ya kupandisha madaraja watumishi 120,0000 na kulipa malimbikizo zaidi shilingi bilioni 1.3.
Ameelekeza waajiri katika sekta za umma na binafsi kuhakikisha maslahi ya wafanyakazi yanazingatiwa hususani katika uandaaji wa mikataba ya wafanyakazi, kutohamisha watumishi bila kulipwa maslahi stahiki,kutenga bajeti na kutoa fursa sawa za kujiendeleza, kuhakikisha pensheni za wafanyakazi zinapelekwa katika mifuko husika kwa wakati, huku akitoa onyo kwa wasimamizi wa utoaji promosheni kutoa promosheni hizo kwa watumishi stahiki na kwa wakati lakini pia kutozuia wafanyakazi wanapotaka kuanzisha amakujiunga na vyama vya wafanyakazi
Aidha amewasihi wafanyakazi kuwajibika katika maeneo yao kwa kujifanyia tathmini kwa kazi walizofanya, kujituma katika majukumu yao na kuweka mbele suala la ubunifu ili kupata matokeo mazuri katika majukumu yao katika ujenzi wa Taifa ili kupata maendeleo, kwani uzalendo, kujituma, ubunifu na matokeo ni njia ya kuleta maendeleo sambamba na kuzingatia uadilifu na kuzingatia maadili katika utumishi wa umma.
Nao wabunge wa majimbo ya Kilosa na Mikumi wamewapongeza wafanyakazi wote kwa namna wanavyoihudumia jamii ambapo wamesema maslahi ya wafanyakazi ni jambo la muhimu ili wafanyakazi waweze kufanya kazi kwa ufanisi huku wakisema Serikali ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ikifanyia kazi changamoto mbalimbali za wana Kilosa ikiwemo utatuzi wa kero ya maji, ujenzi wa nyumba za wafanyakazi, ujenzi wa shule ili kupunguza ongezeko la wanafunzi wanaokaa madarasani kwa wingi, ujenzi na ukarabati wa madaraja, Serikali imetoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa mashine ya mionzi huku wakisema kuwa zipo promosheni na ajira nyingi zinatarajiwa kutolewa sambamba ongezeko la ajira lakini pia wametaka wananchi kutumia fursa ya uzinduzi wa filamu ya Royal tour kujenga hoteli za viwango ili wageni watakaotembelea hifadhi ya Mikumi kufikia hoteli hizo sambamba na kufufua reli ya Kilosa Mikumi Kidatu ambayo itasafirisha watalii kwa njia ya treni.
Wakieleza kilio chao katika maadhimisho ya siku ya Mei Mosi watumishi hao katika risala yao wameainisha vilio vyao hususani katika Mkoa wa Morogoro ikiwemo wafanyakazi kulipwa mishahara duni kima cha chini kikiwa shilingi 80,000 hadi 100,000, kwa mwezi, kutopandishwa cheo/madaraja kwa wakati, baadhi ya waajiri kutoa mikataba isiyofuata sheria na ya muda mfupi kwa kazi endelevu, utatuzi wa migogoro, ucheleweshaji wa kesi za wafanyakazi zinazosajiliwa Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi, matibabu kwa wafanyakazi, malipo ya mikopo ya elimu ya juu.
Changamoto nyingine ikiwa ni kukosa uhuru wa kujiunga na vyama vya wafanyakazi, malipo ya mifuko ya pensheni, ucheleweshaji wa malipo ya kwa wastaafu huku wakiiomba Serikali kuuagiza mfuko wa fidia wa wafanyakazi wanaoumia kazini kulipa wafanyakazi wanaoumia kazini kwa wakati, pamoja na kuutaka mfuko huo kutoa fidia kwa mfanyakazi yoyote anayeumia kazini bila ubaguzi ili mradi mwajiri wake anachangia mfuko huo.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa