Naibu Waziri wa Kilimo Mh. Omary Mgumba mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa kiwanda cha sukari Mkulazi II kilichopo wilayani Kilosa katika kata ya Mbigiri kinachotarajiwa kufungwa mitambo kabla ya mwaka kuisha amewatoa hofu wakulima wadogo na wakati wa miwa kuwa miwa yao haitapotea kwani soko lipo hivyo wasiwe na shaka na mahali pa kuipelekea bidhaa yao ambapo pia amezitaka taasisi za fedha kuendelea kuunga mkono jitihada za kuendeleza mradi huo.
Mgumba amesema Serikali imeadhimia kuongeza mkazo kwenye viwanda vinavyotumia malighafi zinazozalishwa ndani ya nchi ambazo zinatokana na shughuli za kilimo, uvuvi, mifugo, madini na misitu ambapo pia amesema viwanda vyenye soko na mahitaji makubwa ya ndani vitapewa kipaumbele na kiwanda cha sukari ni kimojawapo huku kikifuatiwa na kiwanda cha ngano na mafuta ya kula.
Aidha Naibu Waziri huyo ameishukuru NSSF kwa kufanikiwa kutengeneza barabara ya kutokea Ngerengere mpaka Usungura licha ya changamoto mbalimbali kutokea kama mvua ambayo imeharibu barabara nyingi nchini na kupelekea Serikali kutokuwa na uwezo wa kuzitengeneza zote kwa wakati mmoja lakini pia amemshukuru mkurugenzi wa TARURA kwa kutoa milioni mia mbili kwa ajili ya matengenezo ya barabara ya kutokea Ngerengere mpaka katika shamba la Mkulazi.
Akijibu swali la Naibu Waziri juu ya soko kwa upande wa miwa ambayo ipo tayari kwa matumizi Mtendaji Mkuu wa Mkulazi Selestine Some amesema ununuzi wa miwa ambayo ipo tayari kiwanda cha sukari cha Mtibwa kimeanza kununua miwa kwa wakulima hao licha ya malalamiko ya bei ya kuuza miwa hiyo ambapo mkataba wa awali ulisema miwa itauzwa kwa shilingi 80,000 kwa tani huku Mtibwa wakinunua kwa 60000 kwa tani hii ni kutokana na changamoto za kuchelewa kwa mradi huo na barabara za kwenda shambani kutokupitika ambapo iliwalazimu Mkulazi kuongea na benki ya Azania kusitisha riba ya mkopo uliotolewa kwa wakulima na kukubaliana marejesho kuanza kufanyika mwaka 2021.
Pamoja na hayo Mkurugenzi Mkuu wa NSSF William E. Erio amesema NSSF wanafanya uwekezaji ambao lazima ulete tija na kwamba uwekezaji wa NSSF unafanyika chini ya miongozo ya Benki Kuu ambapo pia ameomba kuwepo kwa elimu kwa wakulima juu ya mikataba inayofanyika ili waweze kuwa na uelewa wa pamoja kwa kuangalia mikataba inajazwa kwa kuzingatia vigezo vya ubora wa bidhaa lakini pia iwepo elimu ya namna ya uzalishaji ili bidhaa zizalishwe kulingana na mahitaji ya viwanda.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi amesisitiza kuwa taarifa za muhimu kuhusu maendeleo ya mradi wa kiwanda cha sukari cha Mkulazi ziwe zinatolewa kwa wakulima ili kuwaondoa hofu kwa kuonyesha jitihada zinazofanyika kwa ajili ya kukamilisha mradi huo, huku Mkurugezi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale akiongeza kusema jitihada zinazofanyika katika kuendeleza mradi huo zifanyike pia katika kutengeneza miundombinu ili eneo la mradi huo liweze kufikika kwa urahisi.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa