Wakala wa barabara vijijini (TARURA) Wilaya ya Kilosa imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 2.5 kwa ajili ya ukarabati wa Barabara yenye urefu wa kilometa 78 kutoka Ruaha mbuyuni hadi kata ya Ulelin`gombe.
Akizungumza wakati wa Mkutano wa Hadhara katika kata ya Uleling’ombe Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Kilosa Badi Noah amesema tayari mchakato umekamilika ambapo kuanzia sasa wataalam wanaanza kufanya upembuzi yakinifu.
Amesema kuwa kata hiyo ipo umbali Zaidi ya kilometa miamoja kutoka makao makuu ya Wilaya hivyo Serikali imeona kuna haja ya kuharakisha zoezi hilo ili Wanananchi waweze kupata huduma ya usafiri na kusafirisha mazao kwenda sokoni.
Noah amesema kuwa Barabara hiyo imekuwa changamoto kwa muda mrefu na wananchi wamekuwa wakipita kwa shida hivyo Serikali imeliona hilo na kutoa kiasi hicho cha fedha kwaajili ya matengenezo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe.Shaka Hamdu Shaka amesema kuwa licha ya Serikali kutoa kiasi hicho cha Fedha kwaajili ya ujenzi wa barabara, Wilaya ya Kilosa ina jumla ya Vijiji 138 na kwamba ifikapo mwishoni mwa mwezi Oktoba 2023, vijiji vyote vitakuwa vimepata umeme kwani mpaka sasa vitongoji 400 vimepata huduma ya umeme kati ya vitongoji 811 vilivyopo Wilayani hapa.
Sambamba na hayo Mkuu wa Wilaya amewataka viongozi wa Vijiji na kata kutoa taarifa kwa Wananchi juu ya mipango ya Serikali katika kutoa huduma kwa wananchi kwani hiyo itapunguza malalamiko.
Kwa upande wake Katibu wa CCM Wilaya ya Kilosa Shabani Mdoe amewataka viongozi wa Chama hicho kusimamia watendaji wa Serikali hususani ngazi ya Vijiji na kata ili waweze kutatua changamoto za Wananchi.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa