Katibu wa Siasa, Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi CCM Taifa Shaka Hamdu Shaka ameagiza Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kuwawesheza vijana kupitia asilimia kumi (10%) ya fedha za mapato ya ndani za Halmashauri kwa ajili ya maendeleo ya Vijana, Wanawake na wenye Ulemavu ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Shaka ametoa agizo hilo Oktoba 4 Mwaka huu akiwa mgeni rasmi katika tukio la uzinduzi wa msimu wa kilimo wa mwaka 2022/2023 uliofanyika kimkoakatika Wilaya ya Kilosa katika Kijiji cha Lukwembe Kata ya Tindiga.
".....Rai yangu sisi tunazo fedha, Vijana hawa lazima wawezeshwe kwa mitaji, Vijana hawa lazima wawekewe utaratibu mzuri wa kusimamiwa, lakini Vijana hawa lazima tuhakikishe kwamba wanaendelea na sio wanarudi nyuma, kuwapa maeneo ni jambo moja, kuwaendeleza ni jambo la pili...."
Aidha, ameongeza kuwa ni wakati wa viongozi kubadilika kimtazamo na kimawazo na badala yake fedha hizo zitumike kwa kuendelezwa kuliko maeneo ambayo fedha hizo zinapotea kutokana na ukosefu wa usimamizi mzuri hivyo madiwani wanao wajibu wa kusimamia fedha hizo ili ziwafikie vijana.
Sambamba na hayo uzinduzi huo umekwenda sambamba na upandaji wa zao la Mkonge katika shamba la vijana lenye ukubwa wa ekari 1,200 kutoka moja ya mashamba 11 yaliyofutwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka kwa kwa wawekezaji na kurejeshwa kwa wananchi ili kupata ardhi ya kulima na kupunguza migogoro baina ya wakaulima na wafugaji ikiwa ni sehemu ya kulifanya zao hilo kuwa la kimkakati.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Morogoro Mh. Fatma Mwassa amebainisha namna Ofisi yake ilivyojipanga kutatua migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji kwani Serikali imedhamiria kujenga Kituo cha Polisi katika katika Kata ya Tindika ambapo Polisi watahusika kwa karibu zaidi kusimamia wakulima na wafugaji ili wafanye shughuli zao bila adha yoyote.
Mwassa amesema shamba la vijana la Ekari 1200 litatumika kulima kwa mfumo wa Block farm na kujikita zaidi kulima zao la mkonge huku eneo nyingine ambalo limeharibiwa na mto Serikali inafanya juhudi kulirejesha ili vijana wengi wapate fursa ya kushiriki kulima mboga mboga na mazao mengine katika eneo hilo kwani lengo la Serikali ni kuzirudisha ekari 3000 zilizoharibiwa na mto hivyo kuwa na jumla ya Ekari 6000 zitakazowawezesha vijana kujiajiri wenyewe na kujikita katika kilimo chenye tija.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kilosa Profesa Palamagamba Kabudi amemshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kufuta umiliki wa mashamba 11 na kuyarejesha kwa wananchi, huku akibainisha kuwa uamuzi huo ni wa kihistoria ambao haujawahi kutokea kufuta idadi kubwa ya mashamba kama hayo kwa wakati mmoja.
Hata hivyo Profesa Kabudi amewataka wananchi wa Wilaya ya Kilosa hususan wa Kata ya Tindiga ambapo mashamba hayo yapo, kutumia fursa hiyo kufanya kazi kwa bidii kwenye kilimo ili kujikwamua kiuchumi kupitia mashamba hayo yaliyofutwa na Mhe.Samia Suluhu Hassan.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa