Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imepokea fedha kiasi cha shilingi bilioni 2.6 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya BOOST, inayolenga kuboresha miundombinu za shule za awali na msingi.
Hayo yamebainishwa Agosti 15, 2025 katika kikao cha maelekezo kilichowakutanisha Walimu wakuu, Watendaji wa kata, Maafisa elimu kata, pamoja na viongozi wa Halmashauri hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Kilosa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Bi. Beatrice C. Mwinuka, akizungumza kwenye kikao hicho, amewataka viongozi kushirikiana kikamilifu kuhakikisha kuwa ujenzi wa miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika ili kutoa huduma bora iliyokusudiwa kwa wananchi.
Bi. beatrice amesisitiza kuwa changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa miradi hiyo zinapaswa kushughulikiwa na kutatuliwa kwa pamoja badala ya kuzigeuza kuwa lawama za mtu mmoja mmoja.
Pia Mkurugenzi huyo amesema kuwa malighafi zote zitakazotumika katika utekelezaji wa miradi hiyo ikiwemo bati, saruji, tails n.k zinunuliwe kwa pamoja viwandani ili kupunguza gharama za fedha ambapo utaratibu huo utasaidia kwa asilimia kubwa kukamilisha miradi yote kwa fedha iliyopo hivyo ameagiza miradi yote ianze kutekelezwa kabla ya msimu wa mvua kuanza ili kuepuka ucheleweshaji zaidi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi wa Halmashauri hiyo Bi. Zakia Fandey amezitaka kamati zinazosimamia ujenzi kuwa imara na kuongeza uwajibikaji, huku akiwataka viongozi kuwa makini wanaposhirikiana na wazabuni kwa kuwa mara nyingi hawana uchungu wa moja kwa moja na mradi.
Naye Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Wilaya ya Kilosa (TAKUKURU) Emily Okelo ametoa onyo kali kwa watakaohusika katika vitendo vya rushwa wakati wa utekelezaji wa miradi, huku akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka taratibu.
Miradi hiyo ya BOOST inatarajiwa kufanya ujenzi na ukarabati wa miundombinu za shule hivyo kuboresha mazingira ya kujifunza na kujifunzia kwa wanafunzi wa awali na msingi.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa