Mradi wa Waridi kupitia Shirika la Sanitation and Water Action (SAWA) umeonekana kuwa mkombozi na mwelimishaji wa masuala ya kujengea watu uwezo lengo ikiwa ni kuhakikisha afya za watu zinaboreka hasa katika sekta ya usafi wa mazingira ikiwemo ujenzi wa vyoo bora, utupaji sahihi wa taka ngumu, unawaji mikono nyakati muhimu pamoja na usafi wa mazingira.
Hayo yamebainishwa na Katibu Tawala Wilaya ya Kilosa Yohana Kasitila wakati wa kufungua kikao cha kurejea mpango wa uendelevu wa mradi na kutoa mapendekezo ya nini kifanyike ili kuhakikisha maisha ya wananchi yanaendelea kuwa bora.
Kasitila amesema kuwa hadi sasa Shirika la SAWA limekuwa msaada mkubwa kwa wilaya kwani maeneo yote yaliyopitiwa na mradi yameonyesha mabadiliko chanya hasa baada ya jamii kuonekana kubadilika baada ya kupata elimu na kuwa bora katika ujenzi wa vyoo bora vinavyosafishika, utupaji taka sahihi pamoja na kuzingatia unawaji mikono kwa nyakati sahihi kwa kutumia vibuyu chirizi.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile. Mwambambale amemwagiza Mkuu wa Idara ya Maji kuangalia kwa kina mema yaliyofanywa na shirika la SAWA ambao muda wa mkataba wao umekwisha baada ya kufanya kazi Kilosa kwa mwaka mmoja ili kuyaendeleza na kuendelea kuihamashisha jamii kuendelea kuifanyia kazi elimu waliyopata na kuendelea kutoa elimu kwa wengine ili elimu hiyo iwe endelevu.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la SAWA Mhandisi Charles Zacharia amesema katika tathmini yao kupitia mradi wamefanikisha uongezeko la ujenzi wa vyoo bora kutoka 35% hadi 45.37%, ongezeko la jamii kunawa mikono nyakati muhimu toka 24.2% hadi 39.92%, ufufuaji wa visima vilivyokufa na uwepo wa wataalam wa kuchukua taarifa za usafi wa mazingira.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa