Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Alhaji Majid Hemed Mwanga amewataka viongozi wote wilayani humo kuwa wabunifu pamoja na kufanya kazi kwa umoja, kushirikiana bila kubaguana wala kudharauliana kwani kwa kufanya hivyo Wilaya itasonga mbele zaidi kimaendeleo.
Majid Hemed Mwanga ambae ameteuliwa na Rais Samia hivi karibuni kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilosa akichukua nafasi ya Alhaji Adam Mgoyi ametoa rai hiyo wakati akijitambulisha ambapo amesema ili kuleta ufanisi katika kazi ni vyema kukawa na ushirikiano, kuheshimiana kwa watumishi wote kuanzia ngazi ya Mwenyekiti wa Kitongoji mpaka ngazi za juu.
Mwanga amesema ili kufanikiwa katika utendaji kazi kila mmoja anawajibika kutoa ushirikiano wa kutosha na kwamba kila mmoja anapaswa kumsemea mema mwenzake badala ya kusemeana mabaya jambo litakalosababisha kutosonga mbele.
Kwa upande wake aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Alhaji Adam Mgoyi amemshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kumteua Alhaji Majid Hemed Mwanga kuwa Mkuu wa Wilaya Kilosa, huku akiwashukuru watumishi, viongozi wa taasisi na wananchi wa Wilaya ya Kilosa kwa ushirikiano waliompa kwa muda wote aliokuwa pamoja nao huku akiwataka kutoa ushirikiano kwa mkuu wa wilaya mpya .
Kwa niaba ya watumishi mwanasheria Tulalemwa Mwenda na meneja wa Mamlaka ya Mapato Kilosa Harun Mussa kwa niaba ya viongozi wa taasisi wamempongeza mkuu huyo wa wilaya kwa uteuzi aliopata huku wakiahidi kuwa wako tayari kushirikiana naye katika majukumu yake lengo ikiwa ni kuifanya Kilosa kukua kimaendeleo.
\
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa