Shule ya Msingi Mikumi mpya iliyopo Kata ya Mikumi Wilayani Kilosa imekabidhi zawadi kwa watoto wabunifu wa Vitu mbalimbali vya kisayansi ikiwa ni mwendelezo wa uibuaji wa vipaji kwa vijana wabunifu wanaosoma shuleni hapo ili kukuza ubunifu wao siku za usoni.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi iliyofanyika Machi 7,2024 Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Ibrahimu Chembe amesema kuwa shule hiyo imepokea kiasi cha Shilingi milioni 1 kwaajili ya kukuza na kuendeleza ubunifu pia uandaaji wa karakana itakayokuwa na vifaa mbalimbali vitakavyosaidia wanafunzi katika suala ubunifu.
Fedha hizo zimetolewa na Tume ya Sayansi na teknolojia (COSTEC) kufuatia Shule hiyo kutoa mshindi wa kwanza kitaifa wa Mashindano ya Ubunifu kwa watoto upande wa shule za Msingi (MAKISATU) kwa mwaka 2022, yaliyoandaliwa na tume hiyo.
Mwalimu Chembe ameongeza kuwa tayari mikakati ya uibuaji na uendelezaji wa vipaji vya ubunifu shuleni hapo unaendelea ambapo mwaka 2023 mwezi Novemba shule iliandaa mashindano kwa wanafunzi ambapo takribani wanafunzi 8 walishiriki na baada ya kuchujwa wamepatikana washidi watatu,Sambamba na hayo amewapongeza washindi hao na kuwataka kuendeleza vipaji vyao ili waweze kufanya vizuri zaidi na kuendeleza vipaji vyao.
Kwa upande wake Afisa Elimu ya Awali na Msingi Bi. Zakia Fandey amesema kuwa huo ni mwanzo tu na kwamba suala hilo litaendelea kufanyika shuleni hapo na amewataka wanafunzi kuendelea kubuni kazi mbalimbali za ubunifu kwani fursa iko wazi kwa kila mwanafunzi.
Aidha amesema kuwa Wilaya itaendelea kupatanua wigo ili shule nyingi zaidi kutoka Kata zote 40 Wilayani hapa ziweze kushiriki kwani anaamini kuna watoto wengi wenye vipaji vya kubuni kazi mbalimbali za kisayansi na kwamba kama watapata nafasi na watu wa kuwaongoza na kuwaelekeza kuna fursa ya kupata kazi nyingine kubwa zaidi ya awali.
Amewataka Walimu kutoa elimu shirikishi kwa kuwapa wanafunzi nafasi ya kueleza wanachokijua kwani watoto wanavitu vikubwa na vizuri hivyo ili kuviona ni lazima walimu waweze kuibua vipaji na kuwa tayari kufundisha kwa vitendo.
Ameongeza wana mpango wa kuandika andiko lingine la kuomba fedha ili kutanua wigo wa ubunifu hivyo amewataka walimu kuwaandaa wanafunzi mapema ili ikifika muda wa mashindano ya ubunifu wanafunzi wawe tayari wameshaandaliwa.
Halmashauri ya Wilaya Kilosa
Sanduku la posta: S.L.P 65 Kilosa
Simu: 023 2623093
Simu: 0737847880
Barua Pepe: ded@kilosadc.go.tz
Hatimiliki imehifadhiwa ©2017 Halmashauri ya Wilaya Kilosa